Naibu Waziri wa katiba na Sheria Bi. Angellah Kairuki akiwa katika mkutano na Wanaharakati wa Kisheria wa Asasi zisizo za Kiserikali ofisini kwake jijini Dar-Es-Salaam.

SERIKALI imeanza mchakato wa uazishwaji wa mfumo wa Wasaidizi wa Sheria (Paralegals) ili waweze kutambulika kwa lengo la kuwawezesha kutoa huduma za kisheria kwa wananchi hasa wa maeneo ya vijijini.

Kauli hiyo imetolewa leo na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Bi. Angellah Kairuki, wakati alipokutana na Wanaharakati wa Kisheria wa Asasi zisizo za Kiserikali ofisini kwake jijini Dar-Es-Salaam.

Mhe. Kairuki amesema kuwa mchakato huo utakapokamilika utawezesha Wasaidizi wa Sheria kutambuliwa na sheria husika na hivyo kupanua wigo kwa wananchi wa mijini na vijijini kuwa na msaada wa kisheria wanapopatwa na matatizo.

“Natambua umuhimu wa uundwaji wa Sheria hii ya Paralegals ndio maana tumeanza mchakato huu kwa kuufanyia marekebisho na kueleza dhana nzima ya Palalegals,” Alisema.

Amewataka Wanaharakati hao kuendelea kuwasisitiza Wasaidizi wa sheria kuhakikisha kuwa wanatoa Huduma zao kwa uwazi zaidi ili wananchi waweze kufaidika hiyo.

Amesema Serikali itahakikisha kuwa inaweka mazingira bora yatakayowawezesha Wasaidizi wa Sheria kufanya kazi zao vizuri lakini kwa kuzingatia misingi ya Sheria na Haki za Binadamu.

Wanaharakati hao wamesema kuwa mpaka sasa Wasaidizi wa Sheria (Paralegals) bado hawajatambulika kisheria na kwamba sheria haitoi nafasi kwa Mawakili wa Serikali au wa kujitegemea kufanya kazi katika Mahakama za Mwanzo na Mabaraza ya Kikata maeneo ambayo ndiyo yenye matatizo makubwa ya kisheria kwa wananchi wa kawaida.

Akizungumza kwenye mkutano huo Wakili wa Kujitegemea Bw. Alphonse Katemi amesema wananchi wengi wanakosa haki kwa sababu mfumo wa kisheria hauruhusu kwa Mawakili kutoa huduma za kisheria katika Mahakama za mwanzo na Mabaraza ya Kata.

“Kwa hiyo ni suala ambalo kwa kweli wananchi wengi wanakosa haki kwa sababu ni mfumo wa kisheria mawakili kwenye mabaraza haya ya ardhi hawaruhusiwi,” Alisema Katemi na kuongeza kuwa huko ndiko kwenye maeneo ambayo yanawatesa sana na kuwaumiza wananchi wa nchi hii.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtandao wa Wasadizi wa Sheria Bi. Flora Masoy amesema kuwa endapo hao Wasaidizi wa Sheria watawezeshwa kutambulika ni wazi kuwa ata kazi zao wanazozifanya nazo zitatambulika kisheria.

Wamesema iwapo Wasaidizi hao watatambulika kisheria itawasaidia kutoa huduma za kisheria hasa kwa wananchi waliopo vijijini ambao ndio wengi wanaokabiliwa na uelewa mdogo wa haki zao.

“Wananchi wengi hasa wa maeneo ya vijijini wanashindwa kupata huduma za kisheria vizuri kutokana na kutokuwepo na watoaji wa kutosha wa huduma za kisheria,” Alisema mmoja wa Wanaharakati.

Naye Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria wa Wizara ya Katiba na Sheria Bw. Joseph Ndunguru, amesema kuwa kwa kutambua umuhimu wa Paralegals Serikali imeandaa Waraka wa Baraza la Mawaziri kwa ajili ya kutunga sheria ambayo lengo kuu kuwatambua Wanasheria Wasaidizi.

Amesema katika mchakato huo wa kuandikwa kwa sheria hiyo Serikali itahakikisha kuwa inawashirikisha wadau mbalimbali katika kupata mawazo mapya yatayowezesha wananchi kupata msaada wa kisheria.

Source:HakiNgowi