MKUU wa wilaya ya Nachingwea,Mkoani Lindi,Bi Regina Chonjo amewataka wananchi wa wilaya hiyo pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo kumpa ushirikiano wa karibu ili aweze kusimamia kwa ukamilifu fursa zilizopo wilayani humo kwa lengo la kuwaletea wananchi maendeleo yao.

Chonjo alisema hayo wakati akizungumza na  waandishi wa habari mara baada ya kuapishwa kuwa mkuu wa wilaya hiyo katika hafla iliyofanyika katika manispaa ya Lindi kwenye ukumbi wa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Lindi.

Mkuu huyo wa wilaya alisema hakuna sababu ya wananchi wa wilaya ya Nachingwea kuendelea kuwa masikini hasa ukizingatia fursa nyingi zilizopo katika wilaya hiyo ikiwa ardhi nzuri isiyohitaji kuwekewa mbolea za viwandani,mvua za kutosha zinazowezakustawisha mazao,misitu na kuwapo kwa madini ya aina mbalimbali ikiwemo Dhahabu na Nikel.

Alisema kuwa atatumia changamoto za mkoa huo zikiwemo za elimu,afya na kilimo kama kipaumbele chake katika kuhakikisha wananchi wanashirikishwa kwenye mipango yote ya maendeleo ili kuwawezesha kuondokana na umaskini.

”Ninayo taarifa kuwa wananchi wa wilaya yangu ni watu wanaopenda kujituma katika shughuli za kuwaletea maendeleo yao ikiwa ni pamoja na kilimo ambacho huwafanya wananchi wa wilaya jirani kutegemea mazao ya chakula kutoka Nachingwea mimi kwa hakika sitawangusha kama iivyompendeza mhe Rais na kuniona ninafaa kumsaidia”

Wananchi hao wameonyesha Jitihada kubwa baada ya Kujenga Ghorofa kwa ajili ya Mkuu wa wilaya hiyo kwa nguvu na pesa zao na kuhakikisha utawala bora unakuwepo .

source:Michuzi