TANGU kutokea kwa vurugu visiwani Zanzibar mwishoni mwa wiki iliyopita ambazo ziliendelea kwa siku nne mfululizo na kusababisha uvunjifu wa amani, uharibifu mkubwa wa mali na hofu kubwa miongoni mwa wananchi, yameulizwa maswali mengi ambayo hadi sasa hayajapatiwa majibu. Moja ya maswali magumu ambayo yamekuwa yakiulizwa na wananchi wengi tangu kutokea kwa vurugu hizo ni kuhusu ukimya wa Rais Muhamed Shein ambaye hadi sasa hajatoa tamko la serikali yake kuhusu vurugu hizo.

Kutokana na hofu kubwa iliyotanda visiwani humo wakati huo na hali ya wasiwasi iliyowakumba wananchi kutokana na vurugu hizo, wengi walitegemea Rais wa Zanzibar, ambaye ndiye kiongozi mkuu wa visiwa hivyo atoe kauli kuhusu vurugu hizo haraka iwezekanavyo. Katika hali hiyo ya sintofahamu, kauli ya Rais Shein ingepunguza hofu na kuwahakikishia wananchi kwamba wasiwe na wasiwasi kwa kuwa serikali yake tayari ilikuwa inachukua hatua za kukomesha vurugu hizo na kuwakamata wahusika wa vurugu hizo.

Hatuna maana kwamba mara baada ya vurugu kuanza Rais Shein angetoa kauli ya kulaani watu au vikundi fulani kwa kuhusika na ghasia hizo kwa sababu ilikuwa mapema mno kwa serikali yake na vyombo vya dola wakati huo kuwatambua wahusika na kuwatia mbaroni. Tunachosema hapa ni kwamba iwapo kauli ya Rais ingetolewa mapema wananchi wangepunguza hofu na wasiwasi na kupata faraja kwamba Serikali ilikuwa imara na ilikuwa tayari inafanya juhudi za kudhibiti hali hiyo. Ukimya wa Rais katika hali hiyo ulionyesha kuwapo ombwe la uongozi, hivyo kusababisha mkanganyiko mkubwa.

Ndiyo maana vurugu ziliendelea hata baada ya kuwasili visiwani humo Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Emmanuel Nchimbi na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Said Mwema na kufanya mazungumzo na viongozi wa dini na vikundi mbalimbali. Haikuwa busara hata kidogo kwa Waziri Nchimbi kwenda visiwani wakati huo kabla Rais Shein hajajitokeza hadharani na kutoa kauli ya kuwathibitishia Wazanzibari kwamba serikali yao ipo imara na tayari imedhibiti hali ya usalama kiasi cha kutosha.

Hivyo ndivyo inavyotokea duniani kote pindi zinapotokea vurugu za kiwango kikubwa kama tulizoshuhudia Zanzibar majuzi. Serikali duniani kote huhakikisha hazifanyi makosa ya kuonyesha kwamba ziko katika hali ya kushindwa kudhibiti mambo pindi matukio kama tuliyoyaona Zanzibar hivi karibuni yanapotokea. Kama tulivyosema hapo juu, katika hali kama hiyo, wakuu wa nchi au serikali hujitokeza haraka na kutoa kauli na taarifa zinazowathibitishia wananchi kwamba serikali husika zipo na zipo imara. Vinginevyo, ni kuacha majeshi ya nchi hizo kupindua serikali halali kwa kisingizio cha kuziba ombwe la uongozi.

Zanzibar inategemea sana utalii kama sekta inayochangia zaidi pato la taifa kuliko sekta nyingine yoyote. Kwa kuzingatia hali hiyo, Rais Shein alipaswa kutambua kwamba kauli yake kuhusu vurugu hizo pia ingewatoa hofu watalii ambao tayari wapo visiwani humo na wengine wanaotegemea kufika siku za baadaye. Lengo la serikali yake siyo tu kuhakikisha sekta ya utalii inakua na kuboreshwa, bali pia inahitaji kuweka mazingira ya utulivu, amani na maridhiano ili watalii wengi zaidi wavutiwe na kutembelea visiwa hivyo kwa wingi.

Katika mazingira ya fujo, chuki, vurugu na umwagaji damu, Wazanzibari wasijidanganye kwamba kuna mtalii yeyote mwenye sifa au vigezo vya kuitwa mtalii atakayethubutu kuhatarisha maisha yake kuja Zanzibar hata kama angekuwa anapenda visiwa hivyo kuliko kitu chochote. Ndiyo maana Serikali ya Kenya imelazimika kuingia vitani na kikundi cha Al Shabab ambacho kimekuwa kikiua na kuteka watalii wanaotembelea nchi hiyo.

Tungependa kumshauri Rais Shein kuwa, ingawa amechelewa sana kutoa kauli juu ya vurugu zilizotokea visiwani humo hivi karibuni, bado anayo nafasi ya kufanya hivyo. Ingekuwa vyema iwapo atatambua kwamba dunia nzima na Wazanzibari wanategemea atoe kauli hiyo sasa, siyo baadaye.

source:Jukwahuru