Yusuph Manji

Hayawi hayawi sasa yamekuwa!!!!!
Taarifa rasmi na za uhakika nilizozipata kutoka makao makuu ya klabu ya Dar Young Africans ni kwamba mwanachama maarufu na tajiri wa klabu hiyo, mfanyabiashara Yusuph Mehebob Manji amechukua fomu za kugombea nafasi ya mwenyekiti wa klabu ya Yanga.

Manji ambaye kwa muda mrefu sasa amekuwa akiisadia Yanga kiuchumi zaidi, nusu saa iliyopita ameenda kwenye makao makuu ya klabu hiyo na kuchukua fomu za uenyekiti bila kuweka wazi kama kwa ajili yake au amemchukulia mtu kwa ajili kugombea nafasi hiyo.

Kwa siku kadhaa sasa kumekuwa na taarifa juu ya Manji kutaka kugombea nafasi hiyo japo mwenyewe bado hajathibitisha, ingawa kitendo chake cha leo kimezidi kuupa nguvu uvumi wa kwamba anataka kugombea nafasi ya kuwa bosi wa Yanga.

Wakati huo huo taarifa nyingine zinasema kuwa aliyekuwa mjumbe Kamati ya Mashindano ya klabu ya Yanga, Abdallah Ahmed Bin Kleb naye muda wowote kutoka sasa atadondoka makao ya Yanga kwa ajili ya kuchukua fomu za kugombea umakamu mwenyekiti.

Mwanachama mwingine maarufu wa klabu hiyo Issac Mazwile naye ameshachukua fomu za kugombea nafasi ya ujumbe wa kamati ya utendaji.