BIASHARA ya dawa za kulevya imeshika kasi mkoani Iringa huku vigogo kadhaa wakitajwa kuhusika, Kwanza Jamii-Iringa linaripoti.

Taarifa zinaeleza kwamba, wafanyabiashara kadhaa maarufu mkoani humo wanatajwa kujihusisha katika usambazaji na utumiaji wa dawa hizo, hususan cocaine, heroin na Mandrax.

Kundi rika la vijana wenye umri kati ya miaka 18 na 35 ndilo linaloongoza kwa biashara hiyo kwa utumiaji na usambazaji, huku bhangi ikiwa inaongoza miongoni mwa orodha ya dawa za kulevya.

“Huwezi kuipiga vita biashara ya dawa za kulevya ikiwa vigogo wenyewe ndio wanaosambaza na kutumia. Wapo wanajulikana, lakini hatujui ni kwa vipi serikali inashindwa kuwakamata,” kimeeleza chanzo chetu cha habari.

Inaelezwa kuwa, wafanyabiashara kadhaa wa mjini humo, ambao baadhi wanadaiwa kuwemo kwenye orodha ya vigogo 58 wa dawa za kulevya iliyopelekwa kwa Rais Jakaya Kikwete mwaka 2006, ndio miungu-watu wanaojificha kwenye mwavuli wa biashara zao halali pamoja na kusaidia jamii.

Taarifa zinaeleza kwamba, vigogo wengi na hasa wenye fedha, ndio watumiaji wakubwa wa dawa za viwandani kama heroin na cocaine kwa vile hawawezi kwenda kununua bhangi mitaani kutokana na hadhi zao, huku kundi kubwa la vijana likitajwa kutumia zaidi bhangi.

Wananchi kadhaa waliohojiwa na gazeti hili kwa masharti ya kutotajwa majina yao, walisema matumizi ya dawa za kulevya mkoani humo yanazidi kushika kasi licha ya serikali kusema yamepungua.

“Huku mitaani sisi ndio tunaowaona watumiaji, wanaongezeka kila wakati na hakuna juhudi za kuwapunguza, hasa vijana ambao wanazidi kuathirika na matumizi hayo,” walisema wananchi hao.

Kauli hiyo ya kukithiri kwa matumizi ya dawa za kulevya iliungwa mkono na Ofisa Mtendaji wa Kata ya Kitanzini iliyo katikati ya Manispaa ya Iringa, Raphael Magata, ambaye alisema matumizi ya dawa za kulevya kwa vijana yanazidi kuongezeka.

Magata alisema kwamba, pamoja na juhudi kubwa zinazofanywa na serikali pamoja na asasi mbalimbali za kijamii kuelimisha juu ya madhara yake, lakini idadi ya vijana wanaojihusisha na biashara hiyo inazidi kuongezeka, hivyo kuitaka jamii ishiriki kupambana ili kuokoa nguvu kazi isipotee.

“Vijana wengi hivi sasa wanajihusisha na utumiaji wa dawa za kulevya ingawa serikali inajitahidi kuwalimisha madhara yake kwa kushirikiana na asasi binafsi. Madhara yake ni makubwa kwa sababu yanachangia pia maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi,” alisema Magata.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Peter Kakamba, alisema kwamba, jeshi lake linajitahidi kupambana na matumizi na biashara ya dawa hizo za kulevya, kwa kushirikiana na jamii kupitia Ulinzi Shirikishi.

Alisema, ushirikiano kati ya jeshi lake na wananchi ni mzuri na ndio uliosaidia kukamatwa kwa kiasi cha debe moja la bhangi katika eneo la Ipogolo katika Manispaa ya Iringa mwishoni mwa mwezi Mei.

“Tunashirikiana vizuri na jamii, lakini vita hii ni ngumu mno, biashara yenyewe inafanywa kwa usiri sana na tunahitaji kuunganisha nguvu za pamoja kati ya jamii na vyombo vya dola, kwani tatizo hili ni letu sote,” alisema.

Kakamba alikiri kuwa dawa za kulevya za viwandani zinatumiwa zaidi na watu wenye fedha, huku akisema matumizi ya bhangi kwa vijana ndiyo makubwa, ingawa alisema wamejitahidi kupunguza kasi ya biashara hiyo kwa kufanya operesheni kadhaa.

Hata hivyo, taarifa mbalimbali zinaonyesha kwamba, Iringa ni miongoni mwa mikoa saba maarufu nchini kwa kilimo cha bhangi, orodha ambayo inahusisha mikoa ya Mara, Arusha, Morogoro, Shinyanga, Mbeya na Ruvuma.

Hali ilivyo nchini

Kwa mujibu wa taarifa za Jeshi la Polisi nchini, kati ya mwaka 2006 na 2010, kumekuwepo na makosa 35,801 ya dawa mbalimbali za kulevya, ambapo kati yao makosa 2,617 yanahusisha dawa za viwandani (cocaine, heroin na mandrax), makosa 30,013 ya bhangi na 3,171 ya mirungi.

Hata hivyo, taarifa ya Hali ya Dawa za Kulevya 2010 iliyotolewa na Tume ya Taifa ya Kudhibiti Dawa za Kulevya inaonyesha kwamba, katika kipindi cha mwaka huo biashara ya dawa za kulevya za viwandani kama cocaine na heroin imeonekana kukua kwa kasi, hali inayodhihirishwa na ukamataji wa kiasi kikubwa cha dawa hizo ikilinganishwa na miaka ya nyuma.

“Ukamataji huu unaashiria wazi kuwa nchi yetu inatumika kupitisha dawa hizo kwenda Kusini mwa Afrika na barani Ulaya. Pamoja na ongezeko hili la ukamataji wa dawa za kulevya za viwandani, bhangi na mirungi zimeendelea kuwa dawa za kulevya zinazopatikana kwa wingi hapa nchini,” imesema taarifa hiyo.

Takwimu za Tume hiyo zinaonyesha kwamba, kati ya mwaka 2000 na 2010, bhangi kavu iliyokamatwa ni tani 2,655.73, ambapo idadi ya kesi zilizofikishwa mahakamani ni 40,877 zikiwahusisha watuhumiwa 46,105.

Kuhusu bhangi iliyosindikwa, takwimu zinaonyesha katika kipindi hicho kiasi cha tani 1,997.4 kilikamatwa kikiwahusisha watuhumiwa 221 ambao walikabiliwa na kesi 58.

Ripoti hiyo iliyosainiwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge) William Lukuvi, pamoja na Kamishna wa Tume hiyo, Christopher Shekiondo, inaonyesha kwamba, katika kipindi hicho kiasi cha tani 68.3 za mirungi zilikamatwa na kesi 4,426 zilifunguliwa mahakamani zikiwahusisha watuhumiwa 4,000.

Aidha, katika kipindi hicho cha mwaka 2000 na 2010, kiasi cha heroin kilichokamatwa kilikuwa kilogramu 349.6 kikiwahusisha watuhumiwa 2,473, ambapo kesi 2,038 zilifunguliwa dhidi yao.

Kwa upande wa cocaine, jumla ya 96.2 zilikamatwa katika kipindi hicho zikiwahusisha watuhumiwa 932 ambao walifunguliwa kesi 894, hii ikiwa na maana kwamba wengi waliokamatwa na dawa hizo ni wale watumiaji wadogo wadogo.

Kuhusu dawa aina ya mandrax (Methaqualone), kiasi kilichokamatwa katika kipindi chote hicho ni kilogramu 314.2 zikiwahusisha watuhumiwa 435, ambapo jumla ya kesi 50 zilifunguliwa dhidi yao.

Changamoto

Jeshi la Polisi linaeleza katika ripoti zake za kila mwaka kwamba, changamoto kubwa inayowakabili katika kupambana na dawa za kulevya ni ukosefu wa rasilimali fedha, ambapo mara nyingi wanashindwa kufanya operesheni, hasa zile za kuteketeza mashamba ya bhangi.

Kwa mfano, mwaka 2010 jeshi hilo liliteketeza jumla ya ekari 296 za bhangi, ambapo kati ya hizo ekari 171 zilikuwa mkoani Mara, 120 mkoani Arusha na ekari tano mkoani Iringa.

Hata hivyo, wananchi mbalimbali wamesema baadhi ya maofisa wa jeshi hilo wasio waadilifu wamekuwa wakishirikiana na wahalifu wa dawa za kulevya, ambapo kila wanapokamatwa huachiliwa licha ya kwamba ushahidi unakuwepo

Source:kwanzajamii