Mwenyekiti wa Chama cha Habari za Michezo nchini (TASWA) Bw. Juma Pinto (katikati)akifafanua nia ya Chama hicho kutaka kuona mwanamichezo bora akipata mafanikio. Kulia ni Katibu Mkuu wa TASWA Amir Mhando na kushoto ni Meneja Mawasiliano wa Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) Imani Lwinga.


Meneja Mawasiliano wa Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) Imani Lwinga akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.


Meneja Mawasiliano wa Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) Imani Lwinga amesema uamuzi wa kutoa fedha una lengo la kumpa uhuru mshindi aweze kufanya mambo anayoyapenda kutokana na zawadi hiyo.

Ameeleza kuwa walipokea ombi kutoka Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), ambacho ndiyo kinaandaa tuzo hiyo, kwamba safari hii kuwe na mabadiliko kwa mshindi akabidhiwe fedha badala ya zawadi ya gari kama ilivyokuwa mwaka jana.

Pia mshindi huyo wa jumla atapewa cheti na kombe.

Lwinga amesema pia Serengeti itatoa zawadi ya Sh. Milioni moja kwa kila mshindi wa michezo mbalimbali ambayo itazawadiwa katika sherehe hizo zitakazofanyika Juni 14 mwaka huu ukumbi wa Diamond Jubilee -Dar es Salaam.

Akizungumzia hilo Katibu Mkuu wa TASWA Amir Mhando amesema wanatarajia wanamichezo mbalimbali watapewa tuzo siku hiyo na kutaja michezo ambayo itapewa tuzo kuwa ni riadha, wavu, netiboli, kuogelea, tenisi, judo, kikapu, soka, ngumi za kulipwa, ngumi za ridhaa,gofu ya ridhaa, gofu ya kulipwa, baiskeli na kriketi.

Michezo mingine ni mpira wa mikono, olimpiki maalum, Mchezaji Bora wa Nje anayecheza Tanzania, Mchezaji Bora Chipukizi, Mchezaji Bora wa Tanzania anayecheza Nje, Karate, Mwanamichezo Bora wa Tanzania mwaka 2011 na Tuzo ya Heshima.

Mhando ambaye pia ni Katibu wa Kamati ya Tuzo amesema Ijumaa watatangaza majina ya wanamichezo wote watakaowania tuzo hiyo na kuipongeza Serengeti kwa udhamini wao wa kila mwaka.

Kwa mujibu wa Mhando mwaka 2006 Mwanamichezo Bora wa Tanzania alikuwa Samson Ramadhan aliyezawadiwa sh. 500,000, wakati mwaka uliofuata mshindi ambaye alikuwa Martine Sulle alizawadiwa Sh.500,000, huku mwaka 2008 mshindi akiwa Mary Naali alizawadiwa sh.750,000.

Wote hao ni wanariadha.

Mshindi wa mwaka 2009 alikuwa mchezaji netiboli Mwanaid Hassan aliyezawadiwa sh. Milioni moja na mwaka 2010 pia alikuwa Mwanaid aliye zawadiwa gari aina ya Toyota Cresta GX 100 .

Akizungumza kwenye mkutano huo, Mwenyekiti wa TASWA Juma Pinto amewashukuru Serengeti na kusema kuwa ana matumaini zawadi hizo zitakuwa kichocheo cha wanamichezo kufanya vizuri zaidi.

source:MOblog