UPELELEZI wa kesi ya mauaji inayomkabili muigizaji nyota wa filamu, Elizabeth Michael maarufu kama Lulu bado haujakamilika.Lulu anakabiliwa na kesi ya mauaji ya msanii mwenzake, Steven Kanumba, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Lakini jana Wakili wa Serikali, Peter Sekwao aliieleza mahakaama hiyo kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuiomba mahakama ipange tarehe nyingine.Hakimu Mkazi, Agustina Mmbando aliahirisha kesi hiyo na hadi Juni 18, 2012 itakapotajwa tena mahakamani hapo.

Hata hivyo, jana mshtakiwa huyo alilazimika kupandishwa kizimbani mara mbili baada ya tarehe ya kutajwa tena kukosewa.

Awali, hakimu Mmbando alisema kuwa kesi hiyo ingetajwa tena Juni 28 kisha mshtakiwa huyo akaondolewa mahakamani na kupelekwa mahabusu akisubiri kurejeshwa mahabusu ya gereza la Segerea.
Lakini baadaye alirudishwa tena mahakamani na kupandishwa kizimbani baada ya kubainika kuwa tarehe iliyopangwa ya kutajwa kwa kesi hiyo haikuwa sahihi kwani karani alikuwa amekosea kuhesababu, ndipo ikapangwa Juni 18.

Jalada hilo lilipelekwa Mahakama Kuu Ijumaa ya Mei 18, mwaka huu baada ya jopo la Mawakili wa mshtakiwa huyo kuwasilisha maombi juu ya uchunguzi kuhusiana na umri halali wa msanii huyo.

Umri wa mshtakiwa huyo umezua utata kama ni mtoto au ni mtu mzima, jambo ambalo limewalazimu mawakili hao kuwasilisha maombi hayo ya uchunguzi wa umri wake Mahakama Kuu.Maombi hayo yaliwasilishwa mahakamani hapo na Wakili Peter Kibatala Mei 15, 2012 na yamepangwa kusikilizwa na Jaji Dk Fauz Twaib Mei 28, 2012.

Mawakili wa mshtakiwa huyo walifikia uamuzi wa kuwasilisha maombi hayo Mahakama Kuu baada ya kugonga mwamba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Kabla ya kuwasilisha maombi hayo Mahakama Kuu, mawakili hao waliwasilisha maombi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Mei 7,2012 wakiiomba iamuru kesi ya msanii huyo isikilizwe katika mahakama za watoto wakidai kuwa bado ni mtoto

source:bongoflavortz