Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa (wa kwanza kushoto), akiteta jambo na mjumbe wa kamati ya maandalizi ya mkutano wa dunia wa Shirika la Roho Mtakatifu, Florentine Mallya na kiongozi wa shirika hilo nchini, Padri Joseph Shio wakati kamati hiyo ilipoenda kupokea zawadi ya ng’ombe wawili ambao wametolewa na rais huyo mstaafu kwa ajili ya wageni wa mkutano huo, shambani kwake Vikawe Bagamoyo Mkoa wa Pwani

Rais mstaafu, Benjamin Mkapa, akiwa na wajumbe wa kamati ya maandalizi ya mkutano wa dunia wa Shirika la Roho Mtakatifu, Padri Florentine Mallya (wa kwanza kushoto), Mkuu wa shirika hilo nchini, PadriJoseph Shio na mjumbe mwingine Philip Ng’oja mara baada ya kuwakabidhi zawadi ya ng’ombe wawili wenye thamani ya ShMilioni 1.4 ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mkutano huo, shambani kwake Chikawe Bagamoyo, Pwani jana

RAIS Mstaafu Benjamin Mkapa ametoa zawadi ya ng’ombe wawili wenye thamani ya zaidi ya Sh Milioni 1.4 kwa ajili ya kitoweo cha wajumbe 15 kutoka nchi 60 duniani ambao watashiriki Mkutano wa Dunia wa Shirika la Roho Mtakatifu (Congregation of the Holy Ghosty), unaotarajiwa kuanza Juni 24 mjini Bagamoyo.
Akizungumza shambani kwake eneo la Vikawe, Bagamoyo mkoa wa Pwani mara baada ya kukabidhi ng’ombe hao kwa kamati ya maandalizi ya mkutano huo ambayo inaongozwa na Padri Joseph Shio, Rais huyo mstaaafu alisema ameguswa kutoa msaada huo kutokana na kulelewa na wamisionari wa shirika hilo.
“Nimekulia katika mikono ya wamisionari wa Shirika la Roho Mtakatifu ambalo lilikuwa linamiliki Shule ya Sekondari Pugu wakati huo ikiitwa St. Francis College kabla haijataifishwa na serikali na sioni kwanini nisitoe kidogo nilicho nacho kufanikisha mkutano huu muhimu” alisema Mkapa.
Alisema Rais huyo mstaafu kuwa licha ya yeye pia kuna wanafunzi wengine ambao walipita Pugu Sekondari ambao nao wamejitolea walicho nacho kuhakikisha mkutano huo wa kwanza kufanyika barani Afrika unafanikiwa.
Mkapa alisema kuwa ng’ombe hao wawili ambao ametoa ni shemu ya zawadi ambazo alipewa na watanzania wakati anastaafu hivyo haoni kwanini asiwatoe zawadi kwa ajili ya shughuli hiyo.
Awali akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, mkuu wa shirika hilo Padri Shio alisema Rais Jakaya Mrisho Kikwete ndie ambaye ataufungua rasmi mkutano huo wa mwezi mmoja hapo Juni 29 mwaka huu.
Alisema mkutano huo pamoja na mambo mengine utajadili lilipotoka shirika, lilipo na litakapokwenda sanjari na changamoto ambazo zinalikabili na kutengeneza dira ya miaka nane hadi 10 ijayo.
Mkuu huyo alisema watendaji wakuu wa shirika hilo wangeweza kuufanya mkutano huo popote lakini wameona umuhimu wa Tanzania na historia ya mji wa Bagamoyo ambako ndipo shirika hilo lilipoingilia mwaka 1868.
“Wamisionari wa shirika waliingia Bagamoyo wakitokea Zanzibar na kuasisi mbegu ya ukatoliki nchini” alisema Shio na kuongeza kuwa shirika hilo linatambulika vema ulimwenguni kutokana na huduma zake kwa wanajamii .
Alisema shirika hilo linatambulika kutoka na jitihada zake za kupiga vita biashara ya utumwa wakati huo kwa kuwanunua na kuwapatia elimu na matibabu wahanga wa biashara hiyo na toka wakati huo shirika hilo limezidi kupanuka nchini na duniani kwa ujuma likitoa huduma za kijamii ikiwa ni pamoja na elimu, afya na masuala ya uchumi.

source:HakiNgowi