WEKUNDU wa Msimbazi Simba kwa kushirikiana na mdhamini wa klabu hiyo Kampuni ya Bia nchini (TBL), leo wametangaza muendelezo wa sherehe za ubingwa wa Ligi Kuu Bara sanjari na mechi za kirafiki katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, iliyoratibiwa na Nationwide Entertainment Center, yenye Makao Makuu Posta Road jijini Mwanza.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye Ukumbi wa Mikutano wa TBL Ilala, Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Simba Ismail Aden Rage (pichani kushoto) alisema kuwa, ziara ya mabingwa hao kanda ya ziwa itakuwa ya siku mbili Juni 16 na 17, ikihusisha mechi mbili za kirafiki ikiwamo dhidi ya Toto Africans – ambayo itatumika kuipongeza Simba kwa kutwaa ubingwa na Toto kwa kubaki Ligi Kuu Bara.

“Tutatoka jijini Juni 15 kwa ndege na Jumamosi Juni 16 tutacheza mechi dhidi ya Toto Africans kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, kabla ya Juni 17 kushuka CCM Kirumba Mwanza kuumana na moja ya klabu kutoka nchini Uganda, ambayo tutawaarifu baada ya kukamilika kwa makubaliano muhimu,” alisema Rage.

Rage aliongeza kuwa, katika ziara hiyo Simba itakuwa na kikosi chake kamili kinachotarajia kucheza Kombe la Kagame, wakiwamo nyota wapya na wa zamani, kutoka ndani na nje ya nchi. Akabainisha kuwa, muda ukiruhusu kabla ya kuanza kwa Kagame, watasafiri mikoa ya Lindi na Mtwara kwa ziara kama hiyo.

“Kikosi kitakachosafiri na hatimaye kucheza Kombe la Kagame, kitakuwa chini ya kocha Milovan Cirkovic ambaye yuko likizo Serbia. Licha ya kumaliza mkataba wake, Milovan atarudi nchini kuendelea na kazi na kama itatokea tukashindwa kumalizana naye, tutasema na kujua nani ataongoza kikosi” alifichua Rage.

Kwa upande wake Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, George Kavishe (pichani kulia), alirudia kuipongeza Simba kwa niaba ya TBL kwa mafanikio yao msimu ulioisha, huku akisema: “Kama wadhamini, tuliziahidi Simba na Yanga mabasi mapya ya wachezaji. Simba itakabidhiwa basi lao siku ya sikukuu yao ‘Simba Day’ inayofanyika Agosti 8, lakini tutaangalia kama Yanga wao watakabidhiwa lini,” alisema Kavishe.

Aliongeza kuwa, kwa kutwaa ubingwa wa bara, Simba itapokea kutoka TBL kiasi cha shilingi mil 25 kama mkataba unavyosema, ambapo Yanga kwa kushika nafasi ya tatu, imepoteza kiasi cha shilingi milioni 15 ambazo ingepata kama ingeshika nafasi ya pili nyuma ya Simba, ambayo hata hivyo imeshikwa na Azam FC.

SOURCE:jaizmelaleo