KIKOSI CHA TWIGA STARS


KOCHA Mkuu wa Twiga Stars, Boniface Mkwasa, amesema kikosi chake kipo fiti kuivaa Ethiopia kutokana na mazoezi aliyowapa wachezaji wake, huku akidai kurejea kikosini kwa Sophia Mwasikili anayecheza soka la kulipwa nchini Uturuki, kutaongeza nguvu.
Mkwasa, kocha wa zamani wa Yanga ambaye timu yake itacheza mchezo huo kesho Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar, ikiwa ni mchakato wa kuwania kufuzu michuano ya Afrika kwa wanawake, amesema anaamini mazoezi aliyowapa yatawapa ushindi.
“Mchezo utakuwa mgumu kwa kuwa Ethiopia nao wapo vizuri na ukumbuke kuwa wapo mbele kwa mabao 2-1 waliyotufunga katika mechi ya awali, bado nina imani kuwa tutautumia vyema uwanja wetu wa nyumbani kuhakikisha tunashinda na kuendelea kusonga mbele.
“Kikosi kipo safi, hakuna majeruhi hata mmoja, wachezaji wanaonyesha hali na morali ya hali ya juu kutokana na kila mmoja kuonyesha nia ya kutaka kushinda.
“Sofia Mwasikili anatarajiwa kuwemo kwenye timu. Nimewapa mazoezi ya kutosha wachezaji wangu, hivyo jukumu la kushinda uwanjani linabaki kwao wenyewe kwa kuwa wao ndiyo wanaocheza uwanjani,” alisema Mkwasa.

SOURCE;globalpublishers