MWANAFUNZI wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Compus ya Mlimani jijini Dar es Salaam, Edda Silyvester, 21, usiku wa kuamkia leo alifanikiwa kutwaa taji la Kitongoji cha Kigamboni City ‘Redd’s Miss Kigamboni City 2012’ katika shindano lililofanyika kwenye ukumbi wa Navy Beach.

Kutokana na ushindi huo Edda alizawadiwa kitita cha Sh. 500,000 taslimu na mgeni rasmi katika shindano hilo, diwani wa Kata ya Kigamboni, Dotto Msawa.

Nafasi ya pili katika shindano hilo lililopambwa na burudani safi kutoka katika bendi ya FM Academia maarufu Wazee wa Ngwasuma ilichukuliwa na Agnes Goodluck ambaye naye alipata zawadi ya Sh. 350,000.

Elizabeth Boniface alichaguliwa kuwa mshindi wa tatu na kupata zawadi ya Sh. 300,000 huku nafasi ya nne ikienda kwa Esther Albert na mshindi watano akiwa ni Khadija Kombo. Elizabeth na Khadija kila mmoja alipata zawadi ya Sh. 200,000.

Jaji Mkuu wa shindano hilo, Benny Kisaka, alitangaza kuwa badala ya warembo watatu atachukua warembo wote watano kwenda kushiriki katika shindano la Kanda ya Temeke baadaye mwaka huu.

Warembo wengine walioshiriki shindano hilo walikuwa ni Sophia Martin, Rosemary Peter, Doreen Kweka na Linnah David waliambulia kitita cha Sh. 150,000 kila mmoja.

Waratibu wa shindano hilo, kampuni ya K& L Media Solutions wanawashukuru wadau wote waliosaidia kufanikisha shindano hilo kwa kufanikisha onyesho hilo ambalo lilikuwa ni la mwisho kwenye kanda ya Temeke.