Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF), Eugen Mikongoti

Ofisa anayeshughulikia Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF),Rehani Athumani


JUMLA ya wanavikundi 400 walio chini ya Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) wameridhishwa na utaratibu wa huduma zinazotolewa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) hatua iliyowafanya kuahidi kujiunga mara moja ili wawe na uhakika wa kupata matibabu.

Hatua hiyo imefikiwa wakati wa mafunzo yaliyotolewa na NHIF kwa wanavikundi hao Dar es Salaamjana ambapo walielezwa faida wanazoweza kupata kupitia utaratibu wa kujiunga na Mfuko huo.Kutokana na hatua hiyo, NHIF kwa kushirikiana na WAMA wataandaa utaratibu utakaowawezesha wanavikundi hao kuanza utaratibu huo mara moja ambao utawanufaisha na kuwapunguzia mzigo wa gharama za matibabu.

Akifungua mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Uendeshaji wa NHIF, Eugen Mikongoti kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu, alisema pamoja na kuwepo kwa changamoto mbalimbali katika sekta ya afya, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya umeendelea kuwa na dhamira ya kuwapatia watanzania wote utaratibu unaoeleweka wa huduma za afya na kuhakikisha wanachama wake wanapata huduma za matibabu kwa heshima inayostahili.

Mafunzo ya wanavikundi hao ni mwendelezo wa mafunzo yaliyotolewa na Mfuko kwa viongozi wa vikundi ambayo yalikuwa na lengo la kuwapa elimu juu ya huduma zinazotolewa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF).

Katika mkutano huo Ofisa anayeshughulikia Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) Rehani Athumani ambaye aliwasilisha mada iliyohusu huduma za matibabu za uchangiaji kupitia NHIF na CHF ikiwa ni pamoja na manufaa yake.

Rehani aliwaeleza wanavikundi hao kuwa endapo watajiunga na Mfuko huo watapata huduma za matibabu katika hospitali zote za Serikali na za binafsi ambazo zimesajiliwa na Mfuko huo.

Alisema kuwa katika kuhakikisha wanachama wa Bima ya Afya hawakumbani na tatizo la ukosefu wa dawa katika vituo vya kutolea huduma, Mfuko pia umesajili maduka ya dawa ambayo mwanachama anaweza kupata huduma ya dawa kama atakosa huduma hiyo katika kituo cha matibabu alichokwenda.

Kutokana na hali hiyo, aliwaomba kujiunga na Bima ya Afya ili wanufaike na mtandao mkubwa wa huduma za matibabu.

Hata hivyo Rehani hakusita kuwakumbusha wajibu wa kuwa walinzi wa huduma za afya hasa pale wanapoona kasoro za kiutendaji katika vituo vya huduma za matibabu.
Kwa upande wa wanavikundi hao, waliweka wazi msimamo wao kuwa wako tayari kujiunga na utaratibu wa Bima ya Afya ili waweze kunufaika na matibabu hatua ambayo itawapa uhakika zaidi wa kuendelea na shughuli zao za uzalishaji kwa kuwa mtaji wa masikini ni afya yake mwenyewe.

Kukubali kwa wanachama hao kujiunga na Bima ya Afya ni moja ya mafanikio makubwa ya WAMA ambayo lengo lake kubwa ni kuhakikisha inawaunganisha wajasiliamali hao na watoa huduma kama Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.

source:jaizmelaleo