Andriy Shevchenko

Mshambuliaji wa Ukraine, Andriy Shevchenko amepanga kustaafu soka la kimataifa baada ya kucheza mechi ya mwisho ya Euro hatua ya makundi dhidi ya England.

Shevchenko, 35, amefunga mabao 48 katika mechi 111 alizocheza katika timu ya taifa ya Ukraine, lakini baada ya timu ya Ukraine kufungwa na England na kutolewa katika mashindano ya Euro 2012, mshambuliaji huyo amesema atastaafu soka la kimataifa.

Alipoulizwa kama mechi dhidi ya England ndiyo itakuwa ya mwisho kwake, Shevchenko alisema, “Hapana natarajia kucheza mechi moja ya mwisho kwa ajili ya kuaga.”

Kuhusu kutolewa kwao katika mashindano ya Euro 2012 Shevchenko alisema, “Tumehuzunishwa sana, kwa sababu tulifanya vizuri katika mechi ya kwanza, ambapo tuliwafunga Sweden, lakini unapokuwa na timu kama England, Ufaransa na Sweden katika kundi moja ujue upo katika kundi gumu sana, tulijitahidi kupambana nao na nadhani tulifanya vizuri ingawa hatukuweza kuingia katika hatua za robo fainali.”

Chanzo: Mpiratz