Bernard Membe
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Tanzania

Tanzania iko tayari kukosa misaada kwa aina yoyote na kuishi maisha ya kujifunga mikanda, lakini siyo kuingia kwenye mtego wa ushoga.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, ambae alisema kwa namna yoyote ya ushawishi, Tanzania haitakuwa tayari kujiinga katika masuala ya kishoga.

“Itakapotokea wahisani wanasitisha misaada kwa sababu ya msimamo wetu, Watanzania tuko tayari kujifunga mikanda na kujibeba wenyewe badala ya kukubali kudhalilishwa utu na utamaduni wetu,” alisisitiza Membe.

Alikuwa akijibu swali la Khatibu Said Haji (Konde-CUF), aliyetaka kujua Tanzania ikiwa ni moja ya nchi zinazopata misaada mbalimbali kutoka kwa mataifa ya nje, imejiandaaje kukabiliana na janga la kuingia katika ndoa za jinsia moja.

Pia mbunge huyo alihoji iwapo serikali itakuwa tayari kuwaeleza Watanzania mikakati jinsi ya kujinasua na mitego hiyo, ikiwamo kuyaelezea mataifa makubwa msimamo wao.

Waziri alisema utamaduni wa Mtanzania na sheria za nchi hazitambui masuala ya ndoa za jinsia moja, hivyo nchi marafiki zikiwamo nchi za Magharibi, zimeendelea kuuheshimu msimamo wa Tanzania.

Chanzo: Mwananchi