Kocha wa football ya Marekani Jerry Sandusky amepatikana na hatia ya kulawiti watoto na huenda akamaliza maisha yake yote yaliyosalia jela.
KoCha huyo msaidizi wa zamani wa timu ya jimbo la Pennsylvania amepatikana na hatia ya makosa 45 kati ya 48 yanayowahusu wavulana 10 katika kipindi cha miaka 15.
Mzee huyo mwenye miaka 68 hakuonesha kushtuka wakati hukumu hiyo ilipokuwa ikisomwa.
Baada ya hapo alirudishwa gerezani ambako atasubiri hukumu ndani ya miezi mitatu.
Waathirika nane wa vitendo vyake walisimama mahakamani kutoa ushahidi dhidi Sandusky waliyedai alikuwa akiwapapasa wakati wa kuoga na kuwalazimisha kuwaangilia kinyume cha maumbile na pia kufanya ‘oral sex’.

Sandusky alikutana na watoto wengi aliowanyanyasha kimapenzi kupitia chama chake cha misaada kwa watoto cha Second Mile ambacho mzee huyo anadai alikianzisha kuwasaidia wavulana waishio katika mazingira hatarishi.

Kocha wa PSU (Pennsylvania State University) Joe Paterno alifukuzwa kazi kwa kutokuchukua hatua za kutosha kufuatia ripoti ya mwaka 2001 kuwa Sandusky alimlawiti mtoto kwenye bafu za PSU.
Paterno alifariki muda mfupi baadaye kwa kansa ya mapafu.