Hili ni swali ambalo nimekuwa nikiwauliza baadhi ya marafiki zangu ambao ni bloggers hivi karibuni. Mwaka mmoja uliopita mtu angeniuliza hili swali ningebaki namshangaa kwa sababu ningeona limekaa kizushi mno lakini tangu nimeingia kwenye ulimwengu wa Digital Marketing nimegundua lazima kila mtu anaemiliki blogger atambue thamani ya blog yake hasa linapokuja suala la blog kuanza kufanya biashara nikimaanisha kupokea matangazo na afanyeje ili thamani isishuke au kuiongeza zaidi. Hii article naiandika kama ushauri baada ya kukutana na kitu ambacho kwa bloggers wengi kinakuwa kikwazo ambacho hawakioni.

Miezi michache iliyopita kampuni yetu ilianza utaratibu wa kukusanya taarifa za blog zote ambazo ziko active kwenye social media bila kujali umaarufu wake na tukazitengenezea kitu kama database, tulipata blog kama 250 ambazo zinapata update walau hata moja kwa siku. Kwa hivi karibuni wateja ambao wanahitaji kutangaza kwenye blog na website nyingi zaidi ambazo hawazifahamu au ni nje ya zile maarufu nikimaanisha tofauti na Jamii Forums, Michuzi, Haki Ngowi, Zoom Tanzania, Bongo Celebrity au 8020 Fashions wameonegezeka. Kilichofuatia baada ya hapo ilikuwa ni kuwasiliana na bloggers mmoja baada ya mwingine ambapo hapo ndipo umuhimu wa hili swali lilijitokeza. Utakuta unamuuliza blogger gharama ya kuweka tangazo kwenye blog yako ni kiasi gani anaweza mfano akakutajia milioni 2, ukimuuliza anatembelewa na watu wangapi anakwambia labda 5,000. Swali hilo hilo ukimuuliza blogger mwingine ambaye anatembelewa na watu 10,000 au 15,000 kwa siku anakutajia laki 5 au laki 7 kwa mwezi.  Unadhani nani hapo atapata dili?  Unaweza kujibu kutumia ile kauli yetu maarufu ya “Hili ni soko huria kila mtu ana bei yake” lakini naomba nikuambie kitu kimoja. Kampuni yoyote ya biashara inayofanya kazi kwa kufuata sheria haiwezi kukubali kukupa wewe wewe mwenye blog yenye wasomaji wachache shilingi milioni moja alafu yule mwenye wasomaji wengi imlipe laki tano. Upo utaratibu unaotumiwa na makampuni wakala “Digital Agency”.

Utaratibu Ulikuwaje/Upoje?

Utaratibu wa zamani  Kampuni kubwa kama Tigo, TBL au Vodacom ilikuwa ikitaka kuweka Tangazo, inaenda kwenye blog inanunua nafasi ya juu kabisa kwenye blog wanamlipa blogger bila kujali hilo Tangazo limeonwa na watu wangapi. Huu utaratibu uliwapagawisha watu wengi ikafikia hatua kila mtu akawa anakimbilia kufungua blog ili apate tangazo la kampuni fulani. Mameneja masoko wa baadhi ya makampuni nao wakachukulia nafasi hii kupiga ulaji, utakuta kule kwenye kampuni anaandika blog moja inachukua milioni tano alafu anakufata wewe blogger ambaye una njaa zako akikutajia laki tano au milioni moja unaona ni nyingi mno unakubali bila kujua unawapa watu faida. Kwa hiyo baada ya baadhi ya makampuni kugundua huu uozo au baadhi kutaka kujua blog zinawasaidia kiasi gani kwenye kampeni zao za kibiashara tofauti na kutangaza matukio ikaonekana kuna umuhimu wa kukikabidhi kitengo cha matangazo ya mtandaoni kwa kampuni wakala wa matangazo

Makampuni Wakala Yanafanyaje Kazi

Kitu cha kwanza kinachoangaliwa ni idadi ya watu wanaoitembelea blog yako, baada ya hapo kinachofuatia mteja wako atataka kujua akiweka Tangazo kwenye blog yako litapata halaiki au litawavutia watu kiasi gani. Kinachofanyika linapowekwa Tangazo kunakuwa na track link ambayo kila mtu anapobofya hilo Tangazo baada ya kulisoma linampeleka kwenye website ya biashara husika au Page yake ya Facebook, Twitter au Blog na inapompeleka kule ile track link inahesabu ni watu kiasi gani wamelibofya. Hapa ndipo makampuni ambayo ni wakala wa mtangazo yanashindwana na bloggers wengi. Kumbuka hawa kila mwisho wa mwezi lazima waipelekee kampuni husika ripoti inayoonyesha impression ya matangazo yao kwenye blogs na websites zenye matangazo yao. Na ili kufanikisha hiki kitu kuna utaratibu wameutengeneza wa kuzifatilia blog zote zinazokubali kufanya nao kazi. Ili ufanye kazi na wakala lazima wawe na uhakika kuwa haitakula kwao.

Kwa ufupi Kampuni hizi ambazo zinajulikana kama Digital Agency ambazo kwetu ndio zinaonekana ni mpya zikitaka kuleta tangazo kwako zitataka kujua:

– Blog yako inatembelewa na watu wangapi kwa siku

– Watu wangapi panga pangua lazima wazame bloguni (Unique visitors)

– Kwa mwezi una wastani wa kupata watu wangapi kwa ujumla

Baada ya hapa zitakutajia nafasi zinayotaka ambazo zinatofautiana bei, nafasi ya juu kabisa ya blog mara zote ina gharama kubwa na zile nafasi za kulia au kushoto gharama inaweza kuwa nusu ya bei na yale matangazo yanayokaa mwishoni (bottom) mara nyingi ni robo ya lile la juu. Kwa yale matangazo ambayo hayami (floater banner) bei yake haipishani sana na yale ya juu (Top banners).

Utapangaje Bei

Bei ya Tangazo lako jitahidi iendane na idadi ya watu ulionao. Kumbuka hizi kampuni zinapoweka Tangazo kwako atategemea watu wabofye tangazo lake na kuna idadi fulani ya clicks atazitaka, mfano tuchukulie blog yako inatembelewa na watu laki moja kwa mwezi,  kampuni itahitaji kupata angalau clicks elfu moja kwenye tangazo husika kwa banner ya juu kabisa na kushuka chini zaidi kwa banner za pembeni na chini kama nilivyokutajia hapo juu.

Unafanyaje Ukipata Tangazo

Tatizo linalojitokeza kwa bloggers wengi ni kuwa akishapata Tangazo anajiona ndio katoka na kuukata. Unatakiwa kujua kuwa linapowekwa Tangazo kwako huo ni msala tayari umenunua, Mteja atataka kuona  hajapoteza hela yake kutangaza kwako kwa hiyo ni wajibu wao kuhakikisha hilo. Usibweteke na kupunguza kuweka vitu vitakavyovutia wasomaji wengi kwenye blog, panga pangua  hakikisha kila siku una vitu vipya. Pia huo ndio muda wa kuanza kuitangaza blog yako kwa nguvu watu waifahamu na kuvuta wasomaji wengi. Njia iliyozoeleka ni kupeleka link Twitter, Facebook au Google+ lakini hakikisha una ushirikiano na bloggers wengine hasa wale wenye watu wengi kukuzidi. Hii njia hata blog inayotembelewa na malaki kama michuzi anaitumia sana. Unaweza kuwa unapost habari kutoka blog nyingine kwa ufupi na mwisho kabisa unaandika kuwa “kwa habari na picha zaidi tembelea link hii.. ikifuatia link ya blog ambayo umeichukua hiyo habari, hiyo itafanya watu watembelee hiyo blog na yule mwenye blog nyingine akiona anapata traffic toka kwako lazima atafanya kitu hicho hicho mwisho wa siku wote mnapiga bao.

Pamoja na yote hayo niliyosema hapo juu, wazungu wanasema “content is the key to any blog” wakimaanisha yale unayoyaweka ndio yataamua hatma ya blog yako. Jaribu kutokuwa mtu wa kuiga wanachofanya watu wengine, kama umeamua kuwa na blog ya matukio hakikisha unakuwa na kitu tofauti kidogo na kile cha Haki Ngowi, Michuzi au Mjengwa. Kama blog yako ni ya Fashion jitahidi sana kufanya vizuri zaidi au tofauti kidogo na Shamimu wa 8020 Fashion au kama ni ya burudani usitake kila kitu chako kifanane na kile DJ Fetty au DJ Choka. Mfano wa blogger ambaye amekuja kitofauti na siku zinavyozidi kwenda anafanya vizuri ni Miriam wa Missie Popular Blog. Kitu anachofanya zipo Blog kongwe kama Bongo Celebrity au 8020 zinakifanya lakini yeye kaongeza ladha ya kuwa exclusive, kitu chochote kipya kinachohusu Fashion au Mastaa nchini siku hizi lazima ukidake kwa MP na anatumia vizuri social media channel kama twitter na facebook kuifanya blog yake iwe na uhai. Sisemi umuige MP ila hata wewe unachotakiwa kufanya ni kufikiria kitu gani blog ambayo wewe unaipenda na imekufanya utamani kuanzisha blog imekikosa kisha kiongeze na kifanye kwa ustadi zaidi.

Kumbuka tunakoelekea itafikia wakati Makampuni na Biashara kubwa kazi ya kujitangaza watazipitisha kwa mawakala. Kwa hiyo ni vizuri ukaufahamu huu utaratibu mapema na ukajipanga hasa kwenye suala la upangaji wa bei na kuhakikisha blog yako inazidi kusomwa ili kuwa na uhakika wa kuwavutia mawakala hawa

source:tanganyikan