Amina Chifupa wakati wa Uhai wake

Habari zilizopatikana jana usiku na kuthibitishwa na mume wake, Bw. Mohamed Mpakanjia, zilisema kuwa Mhe. Chifupa ambaye alikuwa amelazwa katika Hospitali ya Jeshi ya Lugalo jijini Dar es Salaam, alifariki majira ya saa tatu kasorobo, jana usiku.

Mpakanjia alisema kuwa Mhe. Chifupa alikuwa anasumbuliwa na kisukari pamoja na malaria.

Alisema mwili wake unatarajiwa kusafirishwa leo kupelekwa Njombe kwa ajili ya maziko.

`Atazikwa keshokutwa (kesho),`alisema Bw. Mpakanjia kwa njia ya simu.

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Bw. Samwel Sitta, alipopigiwa simu, hakutaka kuzungumzia chochote kuhusu msiba huo mzito.

Mbunge huyo kijana ambaye kitaaluma ni mtangazaji na mwandishi wa habari, alifanikiwa kuingia bungeni katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 kupitia Umoja wa Vijana wa CCM.

Katika kipindi kifupi alichokaa Bungeni, Mhe. Chifupa alijipatia umaarufu mkubwa kutokana na hoja zake nzito katika kutetea maslahi ya vijana na kukemea rushwa.

Na hivi karibuni alitoa mchango muhimu katika mapambano dhidi ya madawa ya kulevya. Inaweza ikawashangaza wengi, kwamba Mhe. Chifupa amefariki, siku ya kilele cha Maadhimisho ya Kupambana na Madawa ya Kulevya Duniani, vita ambayo alikuwa amedhamiria kupambana nayo kwa nguvu zake zote.

Maadhimisho hayo yalifanyika kitaifa mjini Tanga na kuhutubiwa na Rais Jakaya Kikwete.

Mungu ailaze mahali pema roho ya mpendwa wetu Amina Chifupa.

source:bongo5