Vyombo vya habari vya Uingereza vimeripoti kuwa ndege za kivita za nchi hiyo zimejiweka tayari kuishambulia Syria.
Gazeti la Daily Star limeripoti kuwa ndege za kivita za Uingereza ziko katika maandalizi kamili iwapo Uturuki itaamua kuishambulia Syria katika kulipiza kisasi kutunguliwa ndege yake huko Syria. Serikali ya Syria ilitangaza Ijumaa iliyopita kuwa vikosi vyake vya ulinzi viliitungua ndege moja ya Uturuki aina ya Fantom kwa kosa la kuingia katika anga ya Syria kinyume cha sheria. Hii ni katika hali ambayo Rais Abdallah Gul wa Uturuki siku moja baadaye alikiri kuwa ndege hiyo ilikiuka anga ya Syria.
Wakati huo huo ripoti nyingine kutoka Uingereza zinaarifu kuwa wapinzani wa serikali ya Damascus wanapatiwa silaha na vile vile kupewa mafunzo na Uingereza. Katika ripoti yake ya hivi karibuni gazeti la Daily Star limefichua kuwa idara maalumu za anga za Uingereza SAS na maajenti wa M16 wako nchini Syria kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa wapinzani wa serikali na pia kuwapatia silaha.