Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza ametetea hukumu ya maisha dhidi ya mwandishi wa habari wiki jana.
Bw.Nkurunziza ameambia BBC Hassan Ruvakuki alifikishwa mbele ya vyombo vya sheria kama raia aliyevunja sheria na sio kwa misingi ya kazi yake.
Ruvakuki alishtakiwa pamoja na watu wengine 13 kwa makosa ya ugaidi.
Hata hivyo mawakili wake wamesema ameadhibiwa baada ya kufanya mahojiano na kiongozi wa waasi.
Mwandishi wa BBC Erick David Nampesya amezungumza na Rais Pierre Nkurunziza kuhusu miaka 50 ya uhuru wa nchi hiyo kutoka kwa Ubeljiji.
Tangu kuchaguliwa kwake mwaka 2010, serikali ya Burundi imekosolewa na makundi ya kibinadamu ndani na nje ya nchi kwa kuwakandamiza wapinzani wake.
Hukumu dhidi ya mwandishi wa habari Ruvakuki ilizua mshangao mkubwa kote nchini Burundi wakati inapojiandaa kuadhimisha miaka 50 ya uhuru wake.
Mwandishi habari huyo alipatikana na makosa ya kufanya mashambulio mwaka jana katika kijiji kimoja mkoa wa Cankuzo karibu na mpaka na Tanzania. Wapiganaji 14 waliohusika na shambulio hilo waliuawa.
Mawakili wa Ruvakuki wamesema mwandishi habari huyo alikuwa Tanzania kufanya uchunguzi kuhusu kundi jipya la waasi.
Takriban watu laki tatu walikufa nchini Burundi katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vya miaka 12 kati ya jeshi la Wa- Tutsi wengi na wapiganaji wa Ki- Hutu.
Vita hivyo vilimalizika mwaka wa 2005 kufuatia mkataba wa amani na kutoa nafasi ya aliyekua kiongozi wa waasi Pierre Nkurunziza kuchaguliwa kama Rais.