Askari wa polisi wa kituo cha kati mjini Nzega,wakikagua viroba vikubwa vilivyokuwa vimejazwa bangi yenye uzito wa kilogramu 350 na thamani ya shilingi miloni 5,250,000.Bangi hiyo ilikuwa ikisafirishwa na kijana Pascal Bangii mkazi wa kijiji cha Bigiri mkoani Tabora kwenda kuuza Dar-es-salaam.Kijana huyo amehukumiwa kwenda jela miaka 10 baada ya kukiri kosa.

Kijana mkazi wa kijiji cha Sigiri wilayani Nzega mkoani Tabora,Pascal Bangii (31),amehukumiwa na mahakama ya hakimu mkazi mjini Nzega, kwenda jela miaka 10 baada ya kukiri kosa la kusafirisha madawa ya kulevya aina ya bhangi yenye uzito wa kilogramu 350 kupeleka jijini Dar-es-salaam kuuza.

Bangi hiyo uliyokuwa imehifadhiwa kwenye viroba vikubwa vinne na nusu,thamani yake ni shilingi 5,250,000.

Awali mwanasheria wa serikali Maria Mdulungu alidai mbele ya hakimu wa mahakama ya hakimu mkazi,Chiganga Tengwa kuwa mnano juni 29 mwaka huu majira ya mchana katika kituo cha polisi cha kati mjini Nzega,mshitakiwa alikamatwa akiwa na bhangi hiyo akiisafirisha,huku akijua wazi kuwa kitendo hicho ni kinyume na sheria.

Mdulungu alisema siku ya tukio,walipata taarifa kutoka kwa raia wema juu ya kijana huyo kusafirisha bangi ndani ya basi aina ya youtong T.428 BLR mali ya kampuni ya Green stars.

Mdulungu alisema kauli hiyo ya mshitakiwa,iliungwa mkono na kondakta wa basi hilo na baadhi ya abiria, kuwa mzigo huo haramu wa bangi ni mali ya mshitakiwa.

Kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo, Mdulungu aliiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali ili kuwa fundisho kwa mshitakiwa na watu wengine wanaotarajiwa kufanya biashara ya madawa ya kulevya.

Kwa upande wake mshitakiwa,aliiomba mahakama hiyo imwonee huruma kwa madai kuwa anayo familia inayomtegemea na kwamba hilo ni kosa lake la kwanza toka amezaliwa.

Akitoa hukumu hiyo,hakimu Chiganga,alisema mahakama imezingatia maombi yaliyotolewa na pande zote mbili,lakini pamoja na maombi hayo,kosa alilofanya mshitakiwa la kusafirisha baangi ambalo imepigwa marufuku,halivumikili.

“Madawa ya kulevya ikiwemo bhangi,ni hatari sana kwa afya za binadamu na hasa vijana ambao ni nguvu kazi ya taifa.Madawa haya yanapelekea watumiaji kuwa vichaa.Kutokana na ukweli huo,mahakama hii,inakupa adhabu ya kulipa faini ya shilingi 15,250,000 na ukishindwa kulipa faini hii,utakwenda kutumikia jela miaka kumi”,alisema hakimu huyo.

Wakati mwandishi wa habari hii akiondoka mahakamani hapo,mshitakiwa Pascal alikuwa hajalipa faini hiyo na hivyo kulazimika kwenda jela kutumikia kifungo chake.

source:dewjiblog