MUME wa mwanamitindo maarufu Bongo, Jacqueline Patrick, Abdulatif Fundukira (pichani katikati), Jumatatu iliyopita alihenya kusaka dhamana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam na ombi lake kutupiliwa mbali, Risasi Mchanganyiko linahabarisha.
Abdulatif alifikishwa mahakamani hapo akitokea mahabusu katika Gereza la Segerea jijini Dar es Salaam kutokana na tuhuma za kuhusika katika biashara ya madawa ya kulevya.
Mtuhumiwa huyo akiwa na wenzake watano baada ya kupandishwa kizimbani, aliiomba mahakama hiyo impatie dhamana lakini hakimu anayesikiliza kesi hiyo, Riyad Chamshama alimwambia kuwa kulingana na uzito wa kesi yake hawezi kupata dhamana na kumtaka kupeleka madai yake mbele ya sheria kama ataona kuna umuhimu wa kufanya hivyo.
Baada ya kupewa jibu hilo Abdulatif aliiomba mahakama hiyo impatie nakala ya mwenendo wa kesi hiyo kwa ajili ya matayarisho ya kulipeleka shauri hilo mbele ya sheria ili kupata dhamana ambapo aliambiwa atapatiwa wakati kesi hiyo itakapotajwa tena.
Hakimu Chamshama aliihairisha kesi hiyo hadi Julai 16, mwaka huu itakapotajwa tena Mahakamani hapo.
Baadhi ya ndugu, jamaa na marafiki waliofika mahakamani hapo walisikika wakijadili kitendo cha mke wa Abdulatif, Jack Patrick ambaye aliwahi kuingia katika kinyang’anyiro cha kumsaka Miss Tanzania miaka ya nyuma kutoonekana mahakamani hapo.
“Inawezekana kuwa ameamua kumtosa mume wake?” alihoji mmoja wao huku wengine wakisema huenda mlimbwende huyo ametingwa na mambo muhimu.

source:globalpublishers.