Balozi wa Heshima wa mbio za Mt. Kilimanjaro Marathon katika jiji la mapesa la New York City (NYC) nchini Marekani ambaye pia ni mcheza sinema na mlimbwende maarufu kutoka jiji hilo linaloaminiwa kuwa kitovu cha pesa duniani, Mmarekani Deidre Lorenz ameahidi kukisadia kituo cha watoto yatima cha Upendo kilichopo katika Manispaa ya Moshi.

Lorenz alikitembelea kituo hicho siku mbili (tarehe 22 Juni) kabla ya kukimbia mbio za Mt. Kilimanjaro Marathon zilizotimua vumbi tarehe 24 juni mwaka huu kuanzia Moshi Club hadi Rau mudukani.

Mbio za Mt. Kilimanjaro Marathoni zilianzishwa na Marie Frances anayetoka katika jiji la matajiri la Bethesda nje kidogo ya jiji la Washingyon DC nchini Marekani mwaka 1991 baada ya kuombwa na balozi wa zamani nchini Misri.

Marie Frances aliyekuwa muandaaji wa vipindi vya television ya ABC alianzisha mbio za Pyramid Marathon zilizofana sana nchini Misri na kumfanya balozi wa Tanzania nchini Misri wakati ule kumuomba aje Tanzania kuanzisha mbio za marathon.

Mt. Kilimanjaro Marathon ilianzishwa mwaka 1991 katika Manispaa ya Moshi zikiwa ni mbio kukimbia kwa furaha (fun run) inayowaleta wazungu kupanda mlima Kilimanjaro, kukimbia na kwenda kutembelea mbuga zetu za wanyama. Mbio hizi zipo katika kiundi la Seven Continental Marathons ambazo hukimbiwa katika mabara saba ya dunia.

Deidre Lorenz ambaye amewahi kuigiza katika filamu nyingi alipatikana katika bahati nasibu (Raffle) iliyochezeshwa na Mt. Kilimanjaro Marathon 1991 wakati wa mbio za New York Marathon jijini New York Marekani mwaka 2011. Katika bahati nasibu hiyo Deidre Lorenz aliibuka mshindi na kujipatia tiketi ya bure pamoja na gharama za hoteli za kuja kukimbia mbio za Mt. Kilimanjaro Marathon mwaka huu.

Wadhamini wa mbio za Mt. Kilimanjaro Marathon ni kampuni ya ndege ya Ethiopia Airlines (ET) ambayo huwa inantoa tiketi za bei rahisi kwa wale wanaokuja kukimbia mbio hizo. ET pia hugharamia ushiriki wa Mt. Kilimanjaro Marathon 1991 katika mbio za New York Marathon, Boston Marathon na Los Angelos Marathon ili kijitangaza.

Katika mpango huo Mt. Kilimanjaro Marathon 1991 huweka banda la kutangaza vivutio vya Tanzania kama vile mlima Kilimanjaro, mbuga za wanyama, Zanzibar na mali zetu za asili.

Mkakati huu umesaidia sana kuitangaza Tanzania na hivyo kuwapa fursa watalii wengi kutoka Marekani na nchi nyingi duniani kuijua vyema Tanzania. Wengi wa wakimbiaji hawa hutembelea vivutio vya Tanzania baada ya kutembelea banda la Mt. Kilimanjaro Marathon 1991 katika mbio hizo.

Ufadhili wa Deidre Lorenz akishirikiana na taasisi ya Screen Actors Guild utakisaidia sana kituo cha watoto yatima cha Upendo ambacho kinakabiliwa na changamoto nyingi za fedha na vifaa vya kuwatunza watoto wanaolelewa kituoni hapo. Kituo hiki kilianzishwa miaka ya 60 na masista wa shirika la Precious Blood wa Kanisa Katoliki jimbo la Moshi.

Kwa miaka mingi kituo hiki kimekuwa kinapokea watoto wachanga wanaotelekezwa na mama zao baada ya kuzaliwa katika hospitali mbalimbali za mkoa wa Kilimanjaro. Kituo cha Upendo kinawapokea pia watoito ambao mama zao wamefariki wakati wa kujifungua.

Aidha Lorenz ameahidi kuwashawishi walimbwende na wacheza filamu wengine wa Marekani kuja kushiriki katika mbio za Mt. Kilimanjaro Marathon na kutembelea vivutio vya kitalii vya nchi hii kila mwaka.

source:father kidevu