WAZIRI wa Ujenzi, Dk John Magufuli jana aliwasilisha makadirio ya matumizi ya wizara yake kwa mwaka 2012/13 ambayo imetenga fedha kwa ajili ya maandalizi ya ujenzi wa barabara za juu (flyovers), kama moja ya hatua za kupambana na msongamano wa magari jijini Dar es Salaam.Kwa ujumla wake, miradi ya kupunguza msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam thamani yake ni Sh899.063 bilioni, lakini fedha ambazo zimetengwa katika mwaka huu wa fedha ni Sh37.578 bilioni tu sawa na asilimia 4.17 tu ya mahitaji hayo.

Dk Magufuli alisema maandalizi ya ujenzi wa barabara za juu ambayo yametengewa fedha za ndani Sh2 bilioni, unatarajiwa kuanzia katika eneo la Tazara, makutano ya Barabara za Mandela na Nyerere na ujenzi huo utafadhiliwa Serikali ya Japan kupitia shirika lake la misaada (JICA).

Waziri alisema upembuzi wa mradi huo chini ya JICA tayari umekamilika.

“Wizara inaendelea na mpango wa kujenga Flyovers katika Jiji la Dar es Salaam ili kupunguza msongamano. Usanifu katika eneo la makutano ya Barabara ya Mandela na Nyerere umekamilika chini ya JICA na mradi utajengwa na JICA wenyewe mwaka huu wa fedha,” alisema Dk Magufuli

Hata hivyo, Kamati ya Miundombinu ya Bunge ilipinga ujenzi wa flyovers katika makutano ya barabara za Mandela na Nyerere na kueleza kuwa utaongeza tatizo badala ya kulipunguza.

Akiwasilisha maoni ya kamati hiyo, Makamu Mwenyekiti Anne Kilango Malecela, alisema kuwa kama Serikali haitakuwa makini itajikuta ikiongeza tatizo badala ya kuliondoa.

Kamati hiyo ilishauri kuwa Serikali iwe makini na ujenzi wa barabara za juu katika maeneo mengine kwani barabara ikijengwa katika eneo moja inakuwa ni kero kwa maeneo jirani na hivyo kufanya msongamano kuwa ni mkubwa zaidi.

Mikakati mingine
Dk Magufuli aliitaja miradi mingine ambayo inalenga kupunguza msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam kuwa ni pamoja na ujenzi wa barabara za pete (Ring Roads) zenye urefu wa kilometa 98.15.

Alisema mpango huo umetengewa Sh3.273 bilioni ambazo zitatumika kukamilisha kazi zilizobakia katika barabara ya Kituo cha Mabasi Ubungo – Kigogo – mzunguko (roundabout) ya Kawawa – bonde la Msimbazi – makutano ya Twiga na Jangwani.

Pia katika mpango huo wa kupunguza msongamano wa magari jijini Dar es Salaam, Barabara ya Jet Corner – Vituka hadi Devis Corner nayo itakamilishwa.

“Kiasi cha Sh577 milioni kimetengwa kwa ajili ya ukarabati wa barabara ya Ubungo Maziwa – External na Tabata Dampo – Kigogo na Sh1 bilioni kimetengwa kwa ajili ya kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami kwa barabara ya Kimara – Kilungule – External,” alisema Dk Magufuli na kuongeza:

“Sh2 bilioni zimetengwa kwa ajili ya barabara ya Mbezi (Morogoro Road) –Malambamawili (pamoja na barabara iendayo Shule ya Msingi Malambamawili – Kinyerezi – Banana, Sh2.1 bilioni kwa ajili ya barabara ya Tegeta Kibaoni – Wazo Hill – Goba hadi Mbezi na Sh1 bilioni kwa ajili ya barabara ya Tangi Bovu – Goba”.

Alisema Sh577 bilioni zimetengwa kwa ajili ya ukarabati wa barabara ya Kimara – Baruti – Msewe hadi Changanyikeni, wakati ufuatiliaji na usimamizi wa ujenzi wa miundombinu ya mabasi yaendayo kwa kasi (Bus Rapid Transit Infrastructure) umetengewa Sh50 milioni.

Alisema wizara hiyo kupitia Tanroads pia itazihudumia barabara ambazo ziko chini ya wakala huyo wa barabara na kwamba kazi hiyo imetengewa Sh18 bilioni. “Wizara pia ina mpango wa kujenga Dar es Salaam – Chalinze-Morogoro Express Way kwa utaratibu wa Public Private Partnership (PPP),” alisema.

Alisema daraja la Kigamboni limetengewa Sh2.788 bilioni Barabara ya Sam Nujoma Sh 318.36 milioni ambazo zitatumika kulipa sehemu ya malipo ya mwisho ya mkandarasi.

Kwa mujibu wa Dk Magufuli, Barabara ya Kilwa imetengewa Sh8.1 bilioni kwa ajili ya kukarabati na kupanua barabara ya lami kutoka njia mbili hadi nne kati ya Gerezani na Mbagala kwa msaada kutoka Serikali ya Japan na Serikali ya Tanzania.

“Mradi huu unatekelezwa kwa awamu nne ambapo awamu ya kwanza inahusisha sehemu ya Bendera Tatu – Mtoni kwa Azizi Ally, awamu ya pili inahusisha sehemu ya Mtoni kwa Azizi Ally – Mbagala Zakhem, awamu ya tatu inahusisha sehemu ya Mbagala Zakhem – Mbagala Rangi Tatu na awamu ya nne inahusisha upanuzi wa sehemu ya Bendera Tatu – Gerezani,” alisema.

Alisema awamu ya kwanza na ya pili imejengwa kwa msaada wa fedha kutoka Serikali ya Japan na kwamba mkataba wa awamu ya tatu ulisainiwa Oktoba 19, 2010 na umekamilika Mei, 2012.

Alisema katika mwaka wa fedha 2012/13 mradi wa Mbagala Zhakhem – Mbagala Rangi Tatu umetengewa Sh1.5 bilioni zitakazotumika kulipia sehemu ya malipo ya kazi hizo.

“Aidha, kiasi cha Sh6.6 bilioni kimetengwa kwa ajili ya maandalizi ya upanuzi wa sehemu ya Bendera Tatu – Gerezani (Kamata),”alisema.

Kuhusu maegesho ya vivuko Dar es Salaam – Bagamoyo yametengewa kiasi cha Sh2 bilioni na mradi wa ujenzi wa Barabara ya Wazo Hill – Bagamoyo – Msata umetengewa Sh7.396 bilioni na barabara zilizokasimiwa Wizara ya Ujenzi kupitia Tanroads zimetengewa Sh4.398 bilioni.

Mfuko wa Barabara
Kwa mujibu wa Magufuli, katika mwaka wa fedha 2012/13 kiasi cha Sh 300.76 bilioni kutoka Mfuko wa Barabara zitatumika kwa ajili ya kufanya matengenezo ya barabara.

“Kati ya fedha hizo, Wizara ya Ujenzi imetengewa Sh29,775,720,000 na Tanroads Sh 267,981,436,800 huku Bodi ya Barabara ikiwa imetengewa Sh3,007,643,200,’’ alieleza.

Katika hatua nyingine, Waziri alisema kuwa Wizara imetenga jumla ya Sh 420 milioni kwa ajili ya kufanya maandalizi ya ujenzi wa nyumba 10,000 za watumishi wa Serikali katika mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara.

Alisema katika kipindi cha mwaka 2012/13 wizara kupitia Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), imepanga kujenga nyumba 2500 katika mikoa yote Tanzania Bara ambapo jumla ya Sh180 bilioni zitatumika kukamilisha mradi huo.

Jumla ya Sh1,023.033 trilioni ziliombwa na wizara hiyo kwa ajili ya kukamilisha shughuli mbalimbali kwa mwaka wa fedha 2012/13 ambapo fedha hizo ni pamoja na miradi ya maendeleo na matumizi mengineyo.

source:mwananchi