Kocha Mkuu wa Yanga, Tom Saintfiet (kushoto) akifuatilia mazoezi ya timu yake hivi karibuni.

KOCHA Mkuu wa Yanga, Tom Saintfiet ameamua kuwaona wachezaji wake katika hali ya utulivu na mapendekezo ni kuhakikisha kikosi kinajificha nje Tanzania.
Saintfiet raia wa Ubeligiji ametoa pendekezo hilo kwa uongozi wa Yanga na huenda kikosi chake kikaweka kambi katika nchi kati ya Afrika Kusini, Malawi, Ethiopia au nchi nyingine watakayoona ni sahihi.
Kambi hiyo itaanza mara moja baada ya michuano ya Kagame na Yanga kuhakikisha Saintfiet anaweza kuwoana wachezaji katika hali ya utulivu na kufanya tafakari kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu Bara.
“Kweli kocha amesema, lakini tulikuwa na mpango huo tokea awali, ila sasa ni suala la kusubiri nani atakuwa mwenyekiti. Tumepanga iwe baada ya Kagame na baada ya uchaguzi,” kilisema chanzo.
“Kabla ya hapo, timu itaingia kambini angalau siku nne na tumepanga iwe nje ya Dar es Salaam. Halafu kuna mechi moja ya kirafiki dhidi ya JKT Ruvu wiki hii, lengo ni kuendelea kumpa nafasi kocha ili aione timu.”
Kwa upande wa Saintfiet, alisema anataka kikosi kinachocheza kwa kujiamini, pasi za haraka na kasi kama ilivyo kwa Barcelona au Hispania.
“Hapa ni suala la kujifunza na tunahitaji muda, kwa sasa majukumu mengi anayo mwenzangu Fred (anapeleka kidole kwa Minziro). Lakini baada ya Kagame nitakupa majibu na tutaendelea kujifunza.
“Tutahitaji muda lakini nitataka timu inayocheza kwa ushirikiano na kasi kubwa,” alisema Saintfiet.
Mara ya mwisho Yanga kuweka kambi nje ya nchini ni miaka minne iliyopita ilipokuwa chini ya Mserbia, Dusan Kondic. Iliweka kambi nchini Afrika Kusini ambako ilicheza mechi kadhaa za kirafiki na kujiandaa vilivyo.
Saintfiet ametua Yanga kuchukua nafasi ya Kosta Papic raia wa Serbia na ameahidi kuanza kufanya kazi rasmi baada ya michuano ya Kagame.
Hata hivyo, Saintfiet amekuwa akiendelea kufanya kazi ya kukinoa kikosi chake huku akiendelea kukipanga na amesisitiza mechi za kirafiki ingawa inakuwa vigumu kutokana na michuano ya Kagame ambayo wao ni mabingwa watetezi.

source:globalpublishers