Emmanuel Okwi

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Simba, Emmanuel Okwi, raia wa Uganda, ameshindwa kuondoka kwa muda muafaka kuelekea Italia kufanya majaribio katika klabu ya Parma ya nchini humo kutokana na viza yake kucheleweshwa.
Okwi alitarajiwa kuelekea nchini humo kati ya Julai 5 na 6, lakini hadi sasa bado hajaondoka kwa kuwa upatikanaji wa viza umekuwa mgumu.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga, alithibitisha suala hilo na kudai bado viza yake inafuatiliwa katika ofisi za Ubalozi wa Italia nchini Tanzania.
“Okwi bado hajaondoka, jana niliongea naye akasema bado hajapata viza na anaendelea kuifuatilia, kwani imekuwa ikimpa wakati mgumu kidogo kuweza kuipata.
“Anatarajiwa kuondoka mara tu baada ya kuipata ili kwenda kufanya majaribio nchini Italia. Atakaa nchini humo kwa muda wa wiki mbili,” alisema Kamwaga.
Wakati huohuo, Simba imetamba kuwa uwezekano wa mshambuliaji huyo kufuzu majaribio katika klabu hiyo ni wa asilimia 90 kwa mujibu wa taarifa za wakala wake, lakini imesisitiza kuwa hata kama hatafuzu, kuna timu nyingine kutoka Ujerumani imeonyesha nia ya kutaka kumjaribu.

source:globalpublishers