Zaidi ya watu 100 wamekufa Kusini mwa Nigeria baada ya lori lililokuwa limebeba mafuta kulipuka.
Mamlaka nchini humo zimesema kuwa lori hilo lilipata ajali na kuanguka, lakini halikulipuka mara moja, hali iliyowafanya wanavijiji wa karibu na ene la ajali kukimbilia kuchota mafuta, hata hivyo baada ya muda lilipuka na kuwaunguza watu kadhaa.
Mwandishi mmoja wa habari amekaririwa akiiambia BBC kuwa idadi ya vifo inaweza kuongezeka kwa kuwa baadhi ya wakazi wa vijiji vya jirani walikimbia wakiwa wanaungua na kutokomea vichakani.
Matukio ya namna hii yamekuwa yakitokea mara kwa mara nchini Nigeria, ambapo mamia ya watu wamepoteza maisha katika kipindi cha zaidi ya miaka 10 wakijaribu kuchota mafuta yanayomwagika kwenye malori yalipinduka na katika mabomba ya mafuta yanayovuja au yanayokuwa yamehujumiwa.