Home

Ukimwi siyo tishio tena duniani

Leave a comment


WASEMA SILAHA ZOTE ZA KUKABILI VVU WANAZO, WAOMBA FEDHA WAINGIE
WANASAYANSI mbalimbali wanaoendesha tafiti mbalimbali za kutafuta tiba na chanjo ya Ukimwi, wameitangazia dunia kuwa hatua waliyofikia sasa wanauona ugonjwa huo ‘siyo hatari tena’ kwa sababu wanazo silaha zote za kuweza kukabiliana nao.

Ila wakasema, kinachowakwamisha ni ukosefu wa fedha ambazo zinahitajika katika kuendeleza tafiti na kuweka sera mpya za kukabili Virusi Vya Ukimwi (VVU) duniani.

Hayo yalibainika kwenye siku ya pili ya Mkutano wa 19 wa Kimataifa wa Ukimwi unaofanyika mjini Washington DC, Marekani na unahudhuriwa na watu zaidi 22,000 miongoni mwao wakiwamo wataalamu wa afya, watunga sera na wadau wa mapambano dhidi ya ugonjwa huo toka karibu kila kona ya dunia.

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na Kitengo cha Habari cha Mkutano huo na gazeti hili kufanikiwa kupata nakala yake, ilieleza kwamba jopo la wanasayansi nguli duniani walikiri kuwa wamefanyia VVU utafiti wa kutosha ndiyo maana wanatamba kuwa wamefanikiwa katika kuvidhibiti.

“Kwa sasa tunazo silaha zote za kisayansi kumalizia mbali gonjwa hili la Ukimwi. Kilichobaki ni kutumia kikamilifu utaalamu huu katika fursa hii tuliyo nayo,” alisema Rais wa Taasisi ya Kijamii ya Kimataifa ya Mapambano dhidi ya VVU (IAS), Dk Elly Katabira.

Kiongozi huyo ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa Mkutano huo akitokea nchini Uganda, aliongeza: “Kufanikisha hilo ni lazima tukubali kubadili mfumo kwa maana kwamba kuweka sera mpya zitakazowezesha kuokoa kundi linaloathirika zaidi na ugonjwa huu.”

Dk Katabira alifafanua: “Kinachohitajika ni kuweka mfumo utakaowashirikisha wafadhili na watunga sera katika kuweka mpango mzuri wa pamoja tuweza kulimaliza tatizo kwa silaha hizi za kisayansi.”

Naye Mtaalamu wa Tiba katika Chuo Kikuu cha California, Profesa Diane Havlir alisema: “Ujumbe wangu kwenu, hasa kwa watunga sera ni kwamba: endeleeni kuwekeza katika mipango ya kisayansi.”

Kwenye mkutano huo walishiriki pia wanasayansi wenye dawa na ushahidi unaoonyesha kuwa katika miaka ya karibuni zimeonyesha dalili nzuri za kutibu Ukimwi na kifua kikuu (TB).

Wataalamu wengi wa afya waliunga mkono kauli hiyo wakisema kwa sasa kuna uelewa mkubwa wa kitaalamu juu ya muundo na tabia ya VVU hivyo ni rahisi kwao kutengeneza dawa kwa ajili ya kuzuia, kutibu na chanjo.

Tafiti za awali
Kauli ya wanasayansi hao imekuja baada ya miaka 30 ya kipindi kigumu cha kutafiti namna ya kupata chanjo au tiba ya ugonjwa huo ambao umeua mamilioni ya watu duniani, hususan wataalamu na nguvu kazi inayohitajika kuimarisha uchumi.

Waligundua VVU mwaka 1981 na ilikuwa vigumu kupata dawa ya kuviua kwa sababu ya tabia zao na uwezo wa kujigeuza kuwa sehemu ya mwili na kutumia selikinga kuzalisha virusi wengine.

Wanasayansi hao walitoa kauli hizo za matumaini kukabili VVU mbele ya viongozi mashuhuri wa kisiasa, akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Clinton na Rais wa Ufaransa, François Hollande.

Mtaalamu anayesimamia mipango ya afya Ikulu ya Marekani, Profesa Antony Fauci, ambaye piya ni Mkurugezi wa taasisi ya nchi hiyo ya Utafiti wa Magonjwa ya Kuambukiza na Mzio (NIAID), alikuwa miongoni mwa waliohutubia na kusifu hatua iliyofikiwa na wanasayansi duniani.

Ofisa Mkuu na Rais wa Taasisi ya Mapambano ya Ukimwi nchini Marekani, Phill Wilson aliweka bayana kuwa pamoja na ugonjwa huo kuonekana tishio hasa kwa nchi zinazoendelea, hakuna nchi, hata zile tajiri, ambazo zinaweza kutamba haziathiriki na tatizo hilo.

Kwa hivyo akasema mikakati na sera mpya za kisayansi zinahitajika dunia nzima, hivyo akawataka wanasayansi hao ‘kuanika hadharani silaha zao’ ili zianze kutumika ulimwenguni kote.

Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa wa Mapambano ya Ukimwi (UNAIDS), Sheila Tlou aliwataka wataalamu hao kuweka mkakati mzuri utakaowezesha silaha hizo za kisayansi kuelekezwa katika nchi maskini hasa barani Afrika.

Wanasayansi hao wamekuja na kauli hizo za matumaini wakati ambapo tayari wamefanya tafiti mbalimbali na kugundua tabia za VVU ikiwa ni pamoja na vitu ambavyo vinaviwezesha kushambulia seli nyeupe za damu, maarufu kwa jina la CD4, ambazo ni sehemu ya kinga ya mwili wa binadamu.

Licha ya tafiti mbalimbali kuonyesha kuwa kuna kila dalili ya kupatikana kwa chanjo, miaka michache iliyopita, waligundua moja ya dawa zinazotumika kupunguza makali ya VVU (ARV) ijulikanayo kama Truvada, yenye uwezo wa kumkinga mwathirika kumwambukiza mpenzi wanayeshiriki naye tendo la ndoa.

Wiki chache zilizopita, Mamlaka ya Chakula na Dawa ya Marekani (FDA) iliidhinisha Truvada, ambayo ilianza kutumika sehemu mbalimbali duniani tangu mwaka 2004, kuwa ni tiba ya kuzuia kuenea kwa Virusi Vya Ukimwi (VVU).

Kwa mujibu wa maelezo ya FDA, mwathirika anayetumia dawa hiyo anaweza kujamiiana na mwenza wake ambaye hana VVU bila kutumia kondomu na hatomwambukiza.

Matokeo ya utafiti huo wa ARV yaliwahi kuchapishwa kwenye gazeti hili toleo la Februari 12, mwaka huu. Kwa mujibu wa FDA, Truvada inatarajia kuanza kutumika na kusambazwa duniani katika kipindi cha miezi mitatu ijayo

source:mwananchi

MWENYEKITI WA UMOJA WA VIJANA CCM (UVCCM) AUAWA SINGIDA.

Leave a comment


Kamanda wa polisi mkoa wa Singida,Linus Vicent Sinzumwa akizungumza na waandishi wa habari (hawapo kwenye picha) juu ya mauaji yaliyofanywa na wafuasi wa CHADEMA. (Picha na Nathaniel Limu).

Jeshi la polisi mkoa wa Singida, linawashikilia wakazi 18 wa kata ya Ndago jimbo la Iramba magharibi,kwa tuhuma ya kumuua mwenyekiti wa umoja wa vijana CCM (UVCCM),Yohana Mpinga (30) baada ya kumpiga kwa kutumia silaha za jadi.

Kamanda wa Jeshi la polisi mkoa wa Singida, Linus Vicent Sinzumwa alisema tukio hilo la kusikitisha limetokea julai 14 mwaka huu saa kumi alasiri huko katika kijiji cha Ndago.

Alisema siku ya tukio,Chama Cha Maendeleo na Demokrasia (CHADEMA) kilikuwa na kibali halali cha kufanya mkutano wa hadhara katika kijiji hicho cha Ndago na mgeni rasmi katika mkutano huo,alikuwa mbunge wa jimbo la Ubungo jijini Dar-es-salaam.

Sinzumwa alisema mara baada ya CHADEMA kuanza mkutano huo,viongozi wake walianza kuporomosha mvua ya kashifa mbalimbali dhidi ya mbunge wa jimbo hilo Mwingullu Nchemba, kitendo ambacho kiliudhi baadha ya watu waliokuwa wamehudhuria mkutano huo.

“Wananchi hao ambao walichukizwa na kitendo cha kukashifiwa mbunge wao,walianza kupiga kelele kuwa hawataki mbunge wao akashifiwe na badala yake wanataka kusikia sera za CHADEMA tu na si vinginevyo.Hata hivyo,viongozi hao waliendelea tu kuporomosha kashifa dhidi ya Mwingullu na kusababisha kuanza kwa vurugu”,alisema.

Kamanda huyo alisema kuwa vurugu hizo zilihusisha kundi la wanachama wa CHADEMA na wa CCM na zilisambaa.Wanachama hao walianza kurusha mawe ovyo na askari wachache wa polisi waliokuwepo,walizidiwa nguvu na makundi hayo.

“Huyu mwenyekiti wa vijana CCM Yohana,yeye akikimbilia kwenye nyumba ya mwalimu Shume Manase Mpinga ili kuokoa maisha yake,lakini kundi la wananchama wa CHADEMA wakiwa wamebeba fimbo na mawe,walimpiga sehemu mbalimbali za mwili wake na kusbabisha kifo chake papo hapo”,alisema kamanda Sinzumwa kwa masikitiko makubwa.

source:dewjiblog.

HUYU NDIO YULE MWANAFUNZI ALIEANDIKA MISTARI YA BONGOFLEVA KWENYE MTIHANI WA FORM FOUR, HIKI NDICHO ALICHOSEMA.

2 Comments


Julius a.k.a Elinaja.

Unakumbuka February 8 2012 wakati baraza la mitihani lilipotangaza matokeo ya kidato cha nne? stori kubwa ilikua mwanafunzi alieamua kuandika mistari ya bongo fleva kwenye sehemu ya kujibia maswali.

“nashukuru sana wanaosahihisha mitihani hii ya shule yangu, nitakapofeli naendelea na fani yangu ya bongofleva, Majita wangu wako levo za juu na sio East Zuu, kukosa ni kawaida kwa binadamu” hiyo ilikua ni swali namba 6 na 7

kwenye swali la 11 kwenye moja ya mitihani yake aliandika mistari ya bongofleva kwamba “acha utani my girl, unakuja nyumbani umezizi mwenzako huku naona sijiwezi, kazi hiyo ya kuzizi nakwambia ukweli mwanzo ulikua mzuri lakini mwisho ukawa mbaya”

Baada ya hayo matokeo watu wengi ana walitamani kumfahamu huyu mwanafunzi, Jina lake la kuzaliwa ni Julius lakini la kisanii ni Elinaja, na ametoa sababu 5 za kwa nini aliamua kuandika hiyo mistari ya bongo fleva kwenye mitihani yake ya kumaliza kidato cha nne.

Amesema “1 ni kutaka kutuma ujumbe kwa watu wanaosimamia Elimu kwa ujumla, sababu ya pili ni kutaka kusaidia watu wanaoteseka mtaani ambao wanaishi maisha magumu kwa sababu tu ya kushindwa kwendana na system ya elimu iliyopo ambayo ukishindwa kwenda nayo sawa umefeli, tulivyoumbwa kuna mtu anaweza akawa anashindwa kitu flani lakini ni mzuri kwenye kitu kingine sasa mfumo uliopo hautoi nafasi kwa wasioweza hiyo system, sababu ya tatu ni kutokana na utaratibu wa usaishaji wa mitihani kwa sababu sijui kama kuna mwanafunzi yeyote aliewahi kufanya mtihani wake wa mwisho alafu mtihani wake ukarudishwa ili kuona wapi alipokosa na wapi alipopata”

“Sababu ya nne ni kuhusu wazazi kutambua uwezo wa watoto wao toka wakiwa wadogo kipi wanaweza kipi hawawezi ili kuokoa muda na pesa, sababu ya tano ni kwa serikali ijaribu kuweka shule za vipaji toka mwanafunzi akiwa mdogo kabisa, leo hii kuna mtu amepata degree pale chuo kikuu kasoma miaka mitatu na kupewa degree ya sanaa lakini hawezi kukuonyesha cheti hata kimoja kwamba alikua na elimu ya awali ya hiyo degree, huwezi kuniambia una degree wakati hukupata elimu ya msingi ya ulichosomea”

“Kwa namna moja au nyingine sidhani kama nimefanikiwa kwa sababu nilichofanya watu walikichukulia tofauti sikufanikiwa ndio maana nimeamua kujitokeza kumalizia kazi ambayo niliianza kuifanya kule kwa sababu nafsi yangu ilikua inanisuta, ila kwa sasa watu watakua wameelewa na ninaweza kuwasaidia watu wengine” – Julius (Elinaja)

Unaweza kulike au kutweet hii story ili na wenzako wa facebook na twitter waione, shukrani!

source:millardayo

NI LINI SERIKALI ITATIBU CHANZO CHA MGOMO WA MADAKTARI? – ANANILE NKYA

Leave a comment


Katika nchi  yeyote duniani serikali ndiyo  yenye  jukumu la kuweka mazingira mazuri katika hospitali za umma na kuhakikisha kuwamadaktari na wafanyakazi  wa afya  wanafanya kazi yao ya kutibu wagonjwa  kwa  furaha .

Hii  ni kwa sababu serikali  iliyowekwa  madarakani na wananchi moja ya kazi ya   kodi inayokusanya kutoka kwa wananchi   ni kuhakikisha kuwa  hospitali, vituo vya afya na zahanati za umma ziko katika mazingira mazuri na zinatoa huduma nzuri kwa wananchi.

Mazingira mazuri hospitalini ni pamoja na  kuwepo kwa vitanda vya kutosha kwa  wagonjwa,  madawa ya kutosha na ya viwango bora, vifaa kwa ajili ya kupima na kubaini magonjwa na vifaa  na vyumba maalum vya kusaidia watu  wanaofanyiwa upasuaji wasipoteze maisha.

Lakini hali ya hosipitali zetu za umma ni hairidhishi.   Kwa mfano hospitali ya taifa ya   Rufaa Muhimbili ni hospitali  madaktariwanalalamika kuwa hospitali hiyo inakabiliwa na changamoto nyingi ambazo zinawafanya madaktari  kushindwa kutimiza wajibu wao wa  kuokoa maisha ya wagonjwa.

Kwa mfano  hospitali hiyo ina   mashine  ya MRI  ya kupima na kutambua ugonjwa  mbali mbali  kwenye mwili ikiwa ni pamoja na kwenye   ubongo, uti wa mgongo na kifua. 

Lakini  cha kushangaza mashine hiyo  iliyonunuliwa kwa  shilingi zisizopungua Bilioni mbili miaka michache iliyopita,  inapungukiwa kifaa cha bei ndogo  tu cha    kuwezesha  watoto kupimwa. 

Hivyo watoto wenye matatizo yanayohitaji kupimwa kwa mashine hiyo  wanalazimika kupelekwa India au Afrika ya Kusini kwa wale wenye uwezo  wa kujigharamia  vinginevyo kwa maskini walio wengi  huishia  watoto wenye matatizo makubwa yanayoitaji utambuzi wa mashine hiyo, huishia kufa.  

Aidha  madaktari wanalalamika   jinsi wanavyoshindwa kuokoa maisha ya watoto   wanaozaliwa na tatizo la koromeo  la chakula kuungana na koromeo la hewa. Mabingwa wa upasuaji  wa watoto katika hospitali hiyo  wanasema kwa upande wao wanajitahidi kuwafanyia  watoto hao upasuaji, lakini watoto hao huishia  hufariki dunia  kutokana na hospitali hiyo ya Rufaa kukosa  vifaa maalum vya kuhudumia watoto hao na vyumba maalumu vya kuwaweka  baada ya kufanyiwa operasheni.  

“Kinauma sana  na kinakatisha tamaa sana kuona kwamba mtoto anafanyiwa   upasuaji vizuri lakini anapoteza maisha siku chache baadaye kutokana na kukosekana kwa vifaa na mazingira ya kumwezesha  kupona baada ya upasuaji”, anasema  Dakta Catherine Mungo’ngo, Bingwa wa upasuaji wa watoto Hospitali ya Rufaa ya Taifa.

Kwa mujibu wa bingwa huyo kwa mwaka huu pekee watoto watatu  waliozaliwa na tatizo la la koromeo  la chakula kuungana na koromeo la hewa ambao  walifanyiwa upasuaji  Muhimbili,    baadaye  walikufa hospitalini hapo kutokana na kukosekana kwa vifaa vya kuwasaidia kupumulia na chumba maalumu  cha kuwafanyia uangalizi baada ya upasuaji.

Aidha anasema watoto  kati ya 6 hadi 8 wanaohitaji kufanyiwa upasuaji kwa siku, upasuaji huo huahirishwa kutokana na ukosefu wa vifaa , dawa na chumba maalum cha kuwatunzia baada ya upasuaji.

Ni mtu gani mwenye akili timamu  ambaye atafurahia  kuona kazi anayoifanya  haitoi  matunda yanayotarajiwa.?  Ni Daktari gani atakayeendelea kufurajhia kazi yake wakati lengo lake la kuokoa maisha ya watu  linakwamishwa  na  mambo yanayowezekana kurekebishwa?

Daktari furaha yake ni kutibu mgonjwa na kuona anapona. Lakini Daktari katika hospitali za  serikali  atafanyaje kazi yake kuepusha vifo  visivyo vya lazima kama hana vifaa vya kufanyia kazi ?   

Nionavyo mimi,  serikali yetu inapaswa kutafakari tena kwa utulivu na busara kubwa  na kuweka mikakati ya kupata suluhisho la kudumu la mgogoro  wake na madaktari. 

Vinginevyo hata kama wataagizwa  madaktari kutoka Ulaya, na wa hapa nchini kufukuzwa kazi au hata kama viongozi wao ‘watashughulikiwa’,  tatizo la  mazingira ya kazi  hospitalini ambalo ni moja  ya  mambo ya msingi   linalosababisha mgomo wamadaktari   litakuwa halijashughulikiwa  na litaendelea kujirudia  hata kama litapoozwa   kwa mbinu yoyote ile.

 Na ikumbukwe watakaoendelea kuumia zaidi hapa ni wananchi wengi  ambao maisha yao yanategemea uwajibikaji wa serikali yao.

Nijuavyo mimi, serikali  ya wananchi, madaktari wakiwa ni sehemu ya wananchi, husikiliza kero za wananchi na kuzishughulikia badala ya kutumia mabavu na vitisho. 

Mungu ibariki Tanzania.


Ananilea Nkya 

Executive Director 
Tanzania Media Women’s Association (TAMWA) 
P. O. Box 8981, Sinza-Mori 
Dar es Salaam, TANZANIA 
Tel: +255-22 2772681 
Fax +255 22 2772681 

E-mail: ananilea_nkya@yahoo.com
Cellphone:+255-754-464-368

%d bloggers like this: