Home

Tamko Maalum Kutoka CHADEMA Kuhusu Yaliyojiri Katika Mkutano wa Hadhara wa CHADEMA Uliofanyika Kata ya Ndago Siku ya Jumamosi Tarehe 14 Julai 2012

Leave a comment


Ofisa wa Sera na Utafiti CHADEMA Makao Makuu Bw. Waitara Mwita Mwikwabe


CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA)

Tamko Kuhusu Yaliyojiri Katika Mkutano wa Hadhara wa CHADEMA  Uliofanyika Kata ya Ndago Siku ya Jumamosi Tarehe 14 Julai 2012

1. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kiliandaa mikutano ya  hadhara katika Jimbo la Iramba Magharibi. Mikutano hiyo ilitolewa taarifa polisi na jeshi hilo lilitoa baraka zake kama utaratibu wa sheria unavyotaka kwa barua yake ya tarehe 12 Julai 2012 Kumb. Na. KIO/ B1/1/VOL.V/268

2. Mkutano wa kwanza ulipangwa kufanyika katika Kata ya Ndago katika  viwanja vilivyo karibu na kituo cha mabasi ambapo pia ni hatua chache karibu kabisa na Kituo cha Polisi Ndago. Mkutano huu ulipangwa kuanza saa nane mchana.

3. Msafara wa kitaifa unaofanya ziara ya ukaguzi wa chama, katika mkoa  wa Singida chini ya uratibu wa Ofisa wa Sera na Utafiti Makao Makuu, Mwita Mwikwambe Waitara, (ikiwa ni maandalizi ya operesheni nyingine kubwa mkoani humo itakayofanyika baadae), uliwasili katika eneo la  Mkutano majira ya saa tisa na nusu alasiri. Tulikuta wananchi wengi
wakiwa wanatusubiri. Kabla ya Mkutano kuanza tulipewa taarifa kwamba kuna kikundi cha vijana kimeandaliwa kuvuruga mkutano wa CHADEMA kwa kufanya fujo, ikiwemo kurusha mawe ili mkutano huo usifanyike. Suala hilo lilielezwa mkutanoni mapema na Mheshimiwa Waitara, mbele ya askari polisi.

4. Wakati tukijiandaa kuanza hotuba, vijana wapatao wanane walianza chokochoko kwa kutoa matusi na punde mawe yakaanza kurushwa kutoka sehemu mbalimbali. Wakati fujo zinaanzishwa na kile kikundi, Mheshimiwa Waitara alikuwa bado anazungumza na wananchi kuwaandaa kusikiliza wazungumzaji wengine. Vurumai hiyo ilizimwa na wananchi
wenyewe wa Ndago waliokuwa na hamu ya kusikiliza ujumbe wa viongozi wa kitaifa wa CHADEMA.

5. Kwa kweli tunawashukuru wananchi wengi wa Ndago walioonesha ujasiri  mkubwa kuweza kuwaondoa vijana wale eneo la mkutano, kisha mkutano ukaendelea, huku wananchi wakionesha kila hamasa ya kufurahia hoja kutoka kwa wazungumzaji, akiwemo Mheshimiwa John Mnyika, ambaye aliombwa ahudhurie ziara hiyo kwa nafasi yake ya Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CHADEMA.

6. Mpaka tunamaliza mkutano huo ambao wananchi waliufurahia sana kwa  namna ulivyohutubiwa kwa amani na utulivu huku wazungumzaji wakijenga hoja juu ya mstakabali wa jimbo na taifa lao kwa ujumla, mamia ya wananchi waliohudhuria walitaka tuendelea kuhutubia, lakini tulibanwa na ratiba ya kuwahi mkutano wa pili, eneo la Kinampanda.

7. Lakini kutokana na vurugu hizo zilizokuwa zikisababishwa na kikundi  cha vijana ambao tayari ilishatolewa taarifa yao kwenye mkutano huo, lakini askari waliokuwepo hawakuthubutu kuchukua hatua, tulilazimika kuomba msaada kutoka kwa OCD na R.P.C, ambapo baadae wakati mkutano unakaribia kuisha tuliona gari la polisi kutoka Mjini Singida likiwa na askari waliojipanga rasmi kwa ajili ya kuzuia vurugu likifika pale
eneo la mkutano, lakini wakati huo hali ilishatulia na hotuba zimetolewa vizuri.

8. Kutokana na hali hiyo ya vurugu, zilitolewa taarifa Kituo cha  Polisi cha Ndago, ambapo lilifunguliwa jalada NDG/RB/190/2012. Katika jalada hilo tulitaja baadhi ya majina ya watuhumiwa waliokuwa vinara wa kundi lililokuwa likifanya fujo kwenye mkutano mbele ya askari polisi. Majina hayo ni; 1. Daniel Sima, 2. Tito Nitwa, 3. Bakili Ayubu, 4. Yohana Makala Mpande, 5. Ernest Kadege, 6. Abel John, 7. Athuman Ntimbu, 8. Martin Manase, 9. James Ernest, 10. Simion Makacha, 11. Anton John, 12. Frank Yesaya

9. Kwa hakika askari polisi wa Ndago waliokuwepo mkutanoni mbali ya  kutochukua hatua yoyote dhidi ya fujo tulizofanyiwa ikiwemo kupondwa mawe na kikundi kidogo cha wahuni, fujo zilipozidi askari wote walikimbia eneo la mkutano, akabaki OCS pekee ambaye naye alionekana dhahiri kutotaka kuchukua hatua stahili. Hakuonekana kufanya juhudi zozote za kuhakikisha amani inalindwa na ulinzi unaimarishwa katika eneo la mkutano na hatua zinachukuliwa dhidi ya watu walioonekana kudhamiria kufanya fujo.

 Mtu yeyote makini angeweza kuona kuwa askari wale walikuwepo pale mkutanoni ‘almuradi’ tu lakini kama vile walikuwa na maelekezo maalum ya kuhakikisha hawachukui hatua yoyote katika kuzuia mpango wowote wa kusababisha vurugu na kuvunja amani.

10. Baada ya kumaliza mkutano wa Ndago kwa amani, tulikwenda  Kinampanda ambako tulifanya mkutano mwingine mzuri kwa amani kabisa, ambapo mbali ya wananchi kuwa wametusubiri kwa hamu kubwa na kutusikiliza kwa makini hoja zetu, polisi katika eneo hilo walitupatia ushirikiano mzuri tangu wakati tunafika mpaka tulipomaliza mkutano
huo.

11. Jioni wakati tumerudi hotelini, tukasikia kuna taarifa  zinasambazaa kuwa kuna mtu/watu wamekufa katika eneo la Ndago. Habari hizo zilikuwa zinakanganya kwa sababu zilikuwa zikitaja idadi tofauti tofauti. Lakini kwa vyovyote vile kama ni kweli kuna tukio la mtu
kufariki, CHADEMA tunasikitika sana kwa tukio hilo la uhai wa mtu.

12. Tunalaani taarifa zinazozidi kusambazwa ambazo zinawataja polisi  kuwa wanatuhusisha CHADEMA na tukio la mtu aliyefariki. Hii ni ajabu kubwa kwamba tumetoka kwenye mkutano ule kwa amani kabisa mpaka tumemaliza mkutano wa pili kwa amani na polisi wakiwepo sehemu zote mbili, kisha tunasingiziwa masuala ambayo wenyewe hatukuwa na habari nayo tangu mkutano wa kwanza ukiwa unaendelea mpaka mkutano wa mwisho
ulipomalizika.

13. Kutokana na habari hiyo ya kifo cha mtu inavyoenezwa kwa  kuihusisha CHADEMA, tumebaini kuwepo kwa mbinu na mikakati ya chama tawala pia vyombo vya dola vikihusika kutaka kuwatisha wananchi waSingida, Watanzania wote wapenda mabadiliko na viongozi wa CHADEMA katika mkoa huu, wasifanye kazi ya kisiasa kwa kuwabambikizia tuhuma
na kesi na pia kuwafanya waonekane ni watu wa vurugu.

14. Tunapenda kusema hapa kuwa njama hizo hazitafanikiwa. Zitashindwa  kama zilivyoshindwa njama zingine zote ambazo zimekuwa zikifanywa na vyombo vya dola, viongozi wa serikali na chama tawala dhidi ya CHADEMA na vuguvugu la mabadiliko nchini.

15. Tunawataarifu wananchi kuwa ratiba ya kufanya Operesheni nyingine  kubwa katika Mkoa wa Singida, ikiongozwa na Katibu Mkuu, Dkt. Willibrod Slaa, itafanyika baadae kama ilivyoazimiwa na kikao cha Kamati Kuu.


Imetolewa leo Singida, Julai 15, 2012 na;
Waitara Mwita Mwikwabe
Ofisa wa Sera na Utafiti CHADEMA Makao Makuu

source:fatherkidevu

POLISI YAMNASA MTU MMOJA RAIA WA KENYA KWA KUHUSIKA NA SHAMBULIO DHIDI YA DKT. ULIMBOKA.

1 Comment


Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam linamshikilia mtu mmoja raia wa Kenya kwa tuhuma za kuteka nyara na shambulio la kudhuru mwili dhidi ya Dkt. Stephen Ulimboka lilifanyika tarehe 26 Juni 2012. Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Kamanda wa Polisi, Kanda Maalum Suleiman Kova amesema mtu huyo aitwaye Joshua Gitu Mhindi mwenye umri wa miaka 31, ana kitambulisho cha utaifa Na.29166938 kilichotolewa Nyeri na hati ya kusafiria ya dharura Na.0123431 iliyotolewa Namanga Kenya. Kamanda Kova amesema katika mahojiano na polisi mtu huyo alieza kwamba yeye ni mwanachama wa kikundi cha kihalifu kinachojulikana kama GUN STAR chenye makao yake eneo la RUIRU wilaya ya Thika nchini Kenya na kudai kuwa kinaongozwa na mtu mwenye jina la utani SILENCE akisaidiwa na PAST, ambao wamekuwa wakifanya matukio mengi ya kihalifu nchini Kenya.Mtu huyo alipohojiwa zaidi alisema alikuja Tanzania na wenzake 12 kwa lengo la kumdhuru Dkt. Stephen Ulimboka baaada ya kukodiwa na mtu ambaye hakumtaja jina, ambaye anaamini kuwa ni mtumishi wa serikali.Polisi inaendelea na uchunguzi wa tukio hilo ili kubaini wengine waliohusika

‘BLOGGER’ MKONGWE NCHINI ETHIOPIA ESKINDER AHUKUMIWA MIAKA 18 JELA

Leave a comment


Mwandishi wa Habari na ‘Blogger’ kinara nchini Ethiopia Eskinder Nega amehukumia kifungo cha miaka 18 jela kwa kukiuka sheria za nchi hiyo za kukabiliana na ugaidi. Nega na watu wengine 23 walipatikana na hatia mwezi uliopita, ambapo walikuwa wakituhumiwa kujisisha na kikundi kimoja cha upinzani chenye makao yake nchini Marekani kinachoitwa ‘Ginbot Seven’ ambacho serikali ya Ethipia inakichukulia kama kikundi cha kigaidi.Mwezi wa Tano Eskinder alipewa tuzo ya mwaka ya kifahari ya ‘Pen America’s Freedom to Write’ kutokana na kazi zake. Makundi ya Haki za Binadamu yamekuwa yakiikosoa Sheria ya Ethiopia ya Kukabiliana na Ugaidi yakisema haitekelezeki.

WEKUNDU WA MSIMBAZI KUTEMBEZA KOMBE KUANZIA JUNI 16

1 Comment



WEKUNDU wa Msimbazi Simba kwa kushirikiana na mdhamini wa klabu hiyo Kampuni ya Bia nchini (TBL), leo wametangaza muendelezo wa sherehe za ubingwa wa Ligi Kuu Bara sanjari na mechi za kirafiki katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, iliyoratibiwa na Nationwide Entertainment Center, yenye Makao Makuu Posta Road jijini Mwanza.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye Ukumbi wa Mikutano wa TBL Ilala, Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Simba Ismail Aden Rage (pichani kushoto) alisema kuwa, ziara ya mabingwa hao kanda ya ziwa itakuwa ya siku mbili Juni 16 na 17, ikihusisha mechi mbili za kirafiki ikiwamo dhidi ya Toto Africans – ambayo itatumika kuipongeza Simba kwa kutwaa ubingwa na Toto kwa kubaki Ligi Kuu Bara.

“Tutatoka jijini Juni 15 kwa ndege na Jumamosi Juni 16 tutacheza mechi dhidi ya Toto Africans kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, kabla ya Juni 17 kushuka CCM Kirumba Mwanza kuumana na moja ya klabu kutoka nchini Uganda, ambayo tutawaarifu baada ya kukamilika kwa makubaliano muhimu,” alisema Rage.

Rage aliongeza kuwa, katika ziara hiyo Simba itakuwa na kikosi chake kamili kinachotarajia kucheza Kombe la Kagame, wakiwamo nyota wapya na wa zamani, kutoka ndani na nje ya nchi. Akabainisha kuwa, muda ukiruhusu kabla ya kuanza kwa Kagame, watasafiri mikoa ya Lindi na Mtwara kwa ziara kama hiyo.

“Kikosi kitakachosafiri na hatimaye kucheza Kombe la Kagame, kitakuwa chini ya kocha Milovan Cirkovic ambaye yuko likizo Serbia. Licha ya kumaliza mkataba wake, Milovan atarudi nchini kuendelea na kazi na kama itatokea tukashindwa kumalizana naye, tutasema na kujua nani ataongoza kikosi” alifichua Rage.

Kwa upande wake Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, George Kavishe (pichani kulia), alirudia kuipongeza Simba kwa niaba ya TBL kwa mafanikio yao msimu ulioisha, huku akisema: “Kama wadhamini, tuliziahidi Simba na Yanga mabasi mapya ya wachezaji. Simba itakabidhiwa basi lao siku ya sikukuu yao ‘Simba Day’ inayofanyika Agosti 8, lakini tutaangalia kama Yanga wao watakabidhiwa lini,” alisema Kavishe.

Aliongeza kuwa, kwa kutwaa ubingwa wa bara, Simba itapokea kutoka TBL kiasi cha shilingi mil 25 kama mkataba unavyosema, ambapo Yanga kwa kushika nafasi ya tatu, imepoteza kiasi cha shilingi milioni 15 ambazo ingepata kama ingeshika nafasi ya pili nyuma ya Simba, ambayo hata hivyo imeshikwa na Azam FC.

SOURCE:jaizmelaleo