Home

Maafa Ya Kuzama Kwa Meli, Watu 30 wa Fariki dunia mpaka Asubuhii!!

Leave a comment


Na Juma Mohammed,MAELEZO Zanzibar
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imetangaza siku tatu za maombolezo kuanzia Julai 19 hadi Julai 21 kufuatia maafa ya ajali ya Meli ya Mv. Skagit iliyozama karibu na Kisiwa cha Chumbe Zanzibar.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dk. Ali Mohammed Shein akitangaza maombolezo hayo, alisema bendera zote zitapepea nusu mlingoti na kwamba shughuli za sherehe na burudani zimefutwa kwa muda wa siku tatu za maombolezo.

Dk. Shein alisema shughuli za Serikali zitaendelea kama kawaida. Katika taarifa yake aliyoitoa Ikulu usiku wa kuamkia Julai 19, Rais Dk Shein amewahakikishia wananchi na hasa waliopoteza jamaa zao kuwa Serikali itabeba gharama zote za mazishi na pia kugharamia huduma za matibabu kwa majeruhi.

“Nimesikitishwa sana na msiba huu, Katika wakati huu si vema tukaanza kulaumiana jambo la muhimu hivi sasa ni kuokoa maisha ya watu” Alisema Rais Dk. Shein.

Mbali ya taarifa hiyo, Rais Dk Shein aliungana na wananchi, viongozi wa Serikali, vyama vya siasa, Viongozi wa dini katika kutambua maiti zilizofikishwa katika eneo maalum la viwanja vya Maisara Suleiman.

Mbali ya kwenda katika viwanja hivyo, pia alifika katika eneo la bandari ya Zanzibar kufuatilia taarifa za tukio hilo. Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jana lilisitisha shughuli zake kufuatia maafa hayo ambapo wakati wa jioni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Emmanuel Nchimbi alitarajiwa kufanya majumuisho ya bajeti yake.

Baadhi ya Wabunge wakiongozwa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa,Shamsi Vuai Nahodha, Mkuu wa Jeshi la Polisi walitembelea majeruhi katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja pamoja na eneo la viwanja vya Maisara ambapo maiti hufikishwa kwa ajili ya utambuzi.

Mbali ya Bunge, pia Baraza la Wawakilishi Zanzibar jana lilisitisha kwa muda shughuli zake ili kutoa nafasi kwa Wawakilishi hao wa wananchi kushiriki katika shughuli za uokozi ambapo wengi walifika bandarini kusaidia kazi mbalimbali ikiwemo kuwafariji waliopoteza ndugu zao.

Taarifa kutoka Mamlaka za Serikali zinaeleza kwamba hadi asubuhi hii maiti 30 zilipatikana ambapo 20 kati ya hizo zimetambuliwa na kuchukuwa na jamaa zao huku wananchi wengine wakiendelea na kuzitambua maiti zinazofikishwa katika eneo la Maisara.

Aidha, katika taarifa hiyo, watu 145 wameokolewa wakiwa hai, wengi wao wapo katika hali nzuri wameruhusiwa kuungana na familia zao baada ya kupatiwa matibabu katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja Zanzibar.

Meli ya Mv. Skagit ilizama Julai 18,2012 saa 7:50 mchana ikitokea Bandari ya Dar es Salaam kwenda Zanzibar ikiwa imebeba abiria 250 watu wazima, watoto 31 na mabaharia 6.

Kazi ya utafutaji na uokoaji zinaendelea asubuhi hii katika eneo la tukio ilikozama meli hiyo umbali wa maili sita Kusini mwa Kisiwa cha Yasin karibu na Kisiwa cha Chumbe Zanzibar.

Hafla ya Mamlaka ya Hifadhi ya Taifa

Leave a comment


Bodi ya Utalii Tanzania, wiki iliyopita imezindua kampeni ya kutangaza vivutio vya kitalii kwa wageni nchini Australia.
Hafla ya uzinduzi huo uliongoza na mkurugenzi wa bodi bwana Aloyce Kilua na kuhudhuriwa na balozi wa Japan anayewakilisha pia Australia,
New Zealand na Korea Kusini Mh Salome Sijaona, ilifanyika katka hotel ya Novotel mjini Sydney huku wenyeji wa hafla hiyo wakiwa ni
Jumuiya ya Watanzania NSW Australia na kusimamiwa na katibu wake Bw Frank Mtao na Connie Offeh!

Hafla ya Mamlaka ya Hifadhi ya Taifa kuzindua kampeni ya kutangaza vivutio vya kitalii nchini Australia…Picha zaidi zinapatiaka kwenye Jumuiya Tanzanian Community of NSW Australia facebook na website.

“FURSA YENYE TIJA: TAFAKURI YA UTUMISHI WANGU KAMA NAIBU KATIBU MKUU WA UMOJA WA MATAIFA”- DR. ASHA-ROSE MIGIRO.

1 Comment


Hakika kila chenye mwanzo hakikosi mwisho, na kila mwisho wa jambo moja huwa mwanzo wa jingine. Ingawa huenda ni mapema sana kwangu kutoa tafakuri kamili ya muhula wangu katika nafasi ya Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, hapana shaka kabisa kuwa nafasi hiyo imenipa uzoefu maridhawa. Namshukuru Katibu Mkuu BAN Ki-moon kwa kunipa fursa hii, kuniamini na kwa ushirikiano mkubwa wakati wote wa utumishi wangu.

Kukitumikia chombo hiki cha kimataifa kwa muda wa miaka mitano na nusu mfululizo ni heshima ya pekee ambayo daima nitaienzi kama kilele kimojawapo cha maisha yangu ya utumishi wa umma. Kila siku niliyoitumia katika Umoja huo ilikuwa ni darasa la kusukuma mbele mipaka ya ujuzi na elimu. Nimepata kufahamu mengi zaidi kuhusu Shirika lenyewe; kuhusu dunia na watu wake, lakini pia kufahamu ukomo wa uwezo wa Umoja wa Mataifa katika kushughulikia changamoto mbali mbali zinazoikabili dunia yetu.

Utumishi wangu katika Umoja wa mataifa ulikuwa fursa adhimu iliyonipa uzoefu wa pekee. Kazi hii imeujaza moyo wangu na unyenyekevu wa dhati kwani niliingia Umoja wa Mataifa wakati ambapo dunia inachagizwa na madhila makubwa makubwa yakiwemo maradhi, umaskini wa kupindukia, kutokuwapo kwa usawa wa kijinsia, kuongezeka kwa vitendo vya ukatili na udhalilishaji kwa wanawake na watoto; na changamoto nyingine nyingi. Kwa muktadha huu ilikuwa fursa ya pekee kuchangia juhudi za pamoja za kuimarisha Umoja wa Mataifa katika kutekeleza majukumu yake katika kipindi cha mazingira magumu ya kimataifa yaliyojaa changamoto za kipekee kabisa.

Daima nitaendelea kushukuru na kuthamini kwa dhati jinsi Mhe. Rais Jakaya Mrisho Kikwete, Serikali na Watanzania wenzangu walivyonitia moyo na kunienzi katika kipindi chote nilichokuwa Umoja wa Mataifa. Familia yangu, ndugu na marafiki walikuwa karibu nami kwa dua na kunitia nguvu wakati wote wa utumishi wangu. Nawashukuru sana.

Hapana shaka kazi yangu katika Umoja wa Mataifa imeniwezesha kufahamiana kwa karibu na viongozi wengi wa kimataifa na pia watu mbali mbali waliopata mafanikio makubwa duniani. Nimeweza kufahamu kwa undani thamani ya michango yao katika kujenga amani na ustawi wa dunia.

Zaidi ya yote, sitasahau hisia nilizopata kila nilipokutana na watu wanyonge waliokuwa wanahitaji msaada wa Umoja wa Mataifa. Nitakumbuka daima tabasamu ya mwanamke mmoja niliyekutana naye katika moja ya ziara zangu barani Afrika nilipotembelea zahanati mojawapo kati ya kadhaa zinazofadhiliwa na Umoja wa Mataifa. Mama huyo mwenye watoto sita, alikuwa amekikumbatia kitoto chake kimoja kilichokuwa nyonde nyonde; lakini alikuwa na tabasamu iliyojaa faraja na matumaini kwa kuwa alikuwa amefanikiwa kupata bure dawa za kunusuru maisha ya mwanawe.

Maendeleo
 
Nafasi ya Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa iliasisiwa na  Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa  mwaka 1997 kwa madhumuni ya kuongeza ufanisi wa utendaji wa Sekretariati na kuimarisha  uongozi wa Umoja Mataifa katika medani za uchumi na maendeleo ya jamii.  Majukumu ya Naibu Katibu Mkuu yaliongezeka kadri Shirika lilivyokuwa linapanua shughuli zake. Hatimaye Naibu Katibu Mkuu akakabidhiwa jukumu la kuoanisha na kuratibu idara zote zilizo chini ya mwavuli wa Umoja wa Mataifa. Jukumu hili lilikuwa na manufaa makubwa, hususan tulipoingia katika utekelezaji wa dhana ya “Huduma ya Pamoja ” (Delivering as One – DaO) ili kuleta ufanisi zaidi  katika kazi zetu hususan za maendeleo.
Kwa bahati nzuri, ninamaliza kipindi changu kukiwa na maendeleo mazuri yanayotokana na jitihada za kimataifa za kupambana na umaskini. Takwimu za kuaminika za hivi karibuni zinatuambia kuwa juhudi zetu za kupunguza idadi ya watu maskini duniani kufikia angalau nusu ya viwango vya sasa zimeanza kuzaa matunda. Taarifa hii ni ya kutia moyo licha ya ukweli kwamba dunia inapitia dhahama kubwa ya kiuchumi kuliko wakati mwingine wowote katika miaka ya hivi karibuni. Pamoja na majukumu mengine,nguvu zetu tulizielekeza zaidi kwenye kufanikisha malengo ya maendeleo ya milenia na malengo mengine ya maendeleo yaliyokubaliwa kimataifa. Nilihamasika sana na dhamira waliyoionesha wadau na washirika wetu wa maendeleo: serikali, mashirika ya kiraia na mashirika ya biashara. Kwani wote kwa pamoja waliyatumia malengo hayo kama kilingo cha msingi katika kutokomeza umaskini.
Katika kufanikisha utekelezaji madhubuti wa malengo ya maendeleo ya milenia nilipewa jukumu la kukamilisha ahadi ya Katibu Mkuu aliyoitoa kwa nchi wanachama ya kuunda Mfumo Kamilifu wa Utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs Integrated Implementation Framework ). Ninaona fahari kwamba naondoka Umoja wa Mataifa mfumo huu ukiwa umekamilika ambapo Katibu Mkuu aliuzindua mwezi Juni mwaka huu. Kwa mara ya kwanza mfumo huu umeweka utaratibu ambao utauwezesha Umoja wa Mataifa na wadau wote kufuatilia mwenendo wa utekelezaji wa ahadi za kisera na kifedha.  Hapana shaka utaratibu huu utaongeza uwajibikaji wa wadau na upimaji sahihi wa hatua za maendeleo.
Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs) Barani Afrika
 Kwa mwelekeo huo huo,  Katibu Mkuu alizindua Jopo la Viongozi la Kuhimiza Utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Milenia Barani Afrika (MDG Africa Steering Group) mwezi September 2007. Kikundi hiki kinajumuisha taasisi zote kuu duniani zilizo mstari wa mbele katika kuchochea kasi ya maendeleo ya Afrika.  Nilipata bahati ya kukiongoza kikosi-kazi (MDG Africa Working Group) kilichokuwa mhimili wa Jopo hilo la viongozi. Baada ya  miaka mitano ya majadiliano ya kina, Jopo hilo likiongozwa na Katibu Mkuu limetoa mapendekezo kamambe  ya utekelezaji. Endapo mapendekezo haya yatazingatiwa  basi yatakuwa nyenzo muhimu ya kuweka sera na mikakati madhubuti itakayosaidia maendeleo katika nchi husika na duniani kwa ujumla. Napenda kutoa mwito kwa wadau wote kuyapa umuhimu mapendekezo haya.
Ninafahamu kwamba tathmini kamili ya mafanikio ya utekelezaji  wa Malengo ya Maendeleo ya Milenia imepangwa kufanyika Septemba  mwaka 2013.  Hata hivyo tayari tunaweza kusema kuwa Malengo haya yameleta mabadiliko chanya katika maisha ya watu wa kawaida  sehemu nyingi duniani, hususan barani Afrika. Ni dhahiri kuwa jamii  nyingi zimenufaika na utekelezaji wa malengo ya maendeleo ya milenia sio kwa kufanyiwa hisani bali kwa wao wenyewe kuwa na mikakati maalum ya kupiga hatua madhubuti za kujiletea maendeleo stahimilivu na yaliyolenga kuleta usawa baina ya watu.
Mkutano wa Rio + 20
Ni jambo la kutia moyo kwamba maendeleo shirikishi na yenye kuleta usawa ni baadhi ya masuala muhimu yaliyojadiliwa katika mkutano wa Rio +20 uliomalizika hivi karibuni. Suala hili litachukua nafasi kubwa pia katika kuandaa mfumo wa maendeleo unaotarajiwa  baada ya mwaka 2015,  mwaka uliokusudiwa kufikia malengo ya maendeleo ya milenia.  Nilipokabidhiwa jukumu la kuratibu maandilizi ya ushiriki wetu kwenye mkutano wa Rio+20 nilitiwa moyo na nia ya dhati ya mashirika ya Umoja wa Mataifa ya kubuni mkakati wa pamoja wa kutekeleza maazimio ya Rio+20. Napenda kuzishukuru nchi wanachama kwa kufikia makubaliano katika masuala mengi yaliyojadiliwa Rio licha ya changamoto nyingi zinazotokana na mtikisiko wa uchumi duniani. Ninafurahi kwamba maazimio ya mkutano huu yatachangia upatikanaji wa maendeleo stahimilivu, shirikishi na yenye kuleta usawa na hususan kuhakikisha kunakuwa na mustakabali mzuri kwa wanawake na wasichana.
Uwezeshaji wa wanawake na usawa wa kijinsia
Tukirejea kwenye suala hili, hata baada ya Mkutano wa Rio + 20 tutawajibika kuendelea na juhudi za uwezeshaji wa wanawake na kuleta usawa wa kijinsia.  Wakati wa utumishi wangu Umoja wa Mataifa tumefanya bidii kubwa na kutumia muda mwingi kushughulikia suala hii. Tumetumia hadhi na ushawishi wa ofisi yetu kupaza sauti za wanawake na wasichana na kukuza ushiriki wao katika jamii. Tumeendesha kampeni za kupiga vita ukatili kwa wanawake na wasichana.  Tumezihimiza mamlaka katika ngazi za kitaifa na kimataifa kutunga sera na sheria zinazozingatia haki za wanawake na usawa wa kijinsia, na tumetaka wapewe fursa kushika nafasi za uongozi katika jamii.  Ndiyo maana kwa upande wetu hatukuweka koleo chini hadi pale tulipokamilisha uanzishwaji wa idara inayojulikana kwa kifupi kama “UN Women” mnamo Julai 2010. Hii ni idara ya Umoja wa Mataifa  iliyoundwa kwa madhumuni ya kuongoza masuala ya wanawake na usawa wa kijinsia kwa umakini na ufanisi zaidi kuliko hapo awali. Tumefanya jitihada hizi kwa kuamini kuwa hakuna uamuzi wowote ule, uwe mdogo au mkubwa, unaofanywa na Umoja wa Mataifa bila ya kuzingatia maendeleo na ustawi wa wanawake na wasichana.
Huduma ya Pamoja
 
Kwa upande mwingine ninapenda kuwapongeza kwa dhati wenzangu wote waliomo katika utumishi wa Umoja wa Mataifa,wake kwa waume,walioutumia ujuzi na weledi wao wote kuchangia maendeleo ya nchi na jamii tunazozihudumia. Natoa shukrani za pekee kwa wale wote waliopo kwenye ofisi na vituo vya Umoja wa Mataifa nje ya Makao Makuu na ambao wanafanya kazi katika mazingira magumu na yenye changamo nyingi. Hao wote wanadhihirisha umuhimu wa kuwapo kwa Shirika hili kama chombo cha kuhimiza maendeleo katika ngazi zote za kitaifa, kikanda  na kimataifa. Katika kutekeleza dhana ya “Huduma ya Pamoja” (Delivering as One) Waratibu Wakaazi wa Umoja wa Mataifa wamekuwa na mchango muhimu sana.Uratibu wao umeongeza ubora na wepesi wa utoaji huduma kwa nchi wanamowakilisha Shirika. Hatuna budi kuwashukuru kwa mchango wao mkubwa katika kufanikisha dhana ya “Huduma ya Pamoja”.  Ni dhahiri kwamba  uwezo wa nchi mwanachama kumiliki mchakato wa maendeleo yake unakuwa  imara zaidi  pale ambapo kuna mtiririko mzuri wa huduma za Umoja wa Mataifa na fursa za kukuza ushirikiano endelevu na wadau wengine wa maendeleo.  Wakati uamuzi rasmi kuhusu maendeleo ya dhana hii ukisubiri kukamilika kwa majadiliano ya nchi wanachama, ninaamini kwa dhati kuwa utaratibu wa kutoa  “Huduma ya Pamoja” kupitia mpango mmoja uliokubaliwa na wote ni mwelekeo sahihi na wenye tija.
Nchini mwetu Tanzania, mashirika ya Umoja wa Mataifa yamekuwa yakifanya kazi kwa ushirikiano wa karibu sana toka mwaka 2011 kupitia mpango mmoja uitwao “Mpango wa Umoja wa Mataifa wa Kusaidia Maendeleo” (United Nations Development Plan – UNDAP). Mpango huu unakwenda sambamba na mwaka wa fedha wa Serikali yaani Julai 1 hadi Juni 30 na kwa mantiki hiyo kuuwezesha kuzingatia vipaumbele vya Serikali. Kupitia mpango huu Umoja wa Mataifa umejiwekea utaratibu wa kujipima na kujitathmini ambao unatoa fursa kwa hatua za haraka kuchukuliwa inapobidi. Utaratibu huu unapatikana kwenye tovuti. Kwa upande wa uendeshaji, mfumo huu wa utendaji kazi kwa pamoja umetuwezesha kutekeleza majukumu mengi kwa kutumia raslimali chache ambapo“ziada” iliyopatikana imeelekezwa kwenye shughuli nyingine za maendeleo.
Afya ya Jamii
Katika eneo la afya, ambamo wanawake na watoto ndiyo wanaathirika zaidi, hatua muhimu zinachukuliwa kupunguza vifo na kuhakikisha kwamba kila mwanamke na kila mtoto anakingwa na maradhi, hususan kuzuia maambukizi ya virusi vya UKIMWI kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.  Tukiwa Nairobi Aprili mwaka 2011, Katibu Mkuu Ban Ki-moon, Michel Sidibe, Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia UKIMWI (UNAIDS)  pamoja nami tulishuhudia mfano hai wa jitihada za Umoja wa Mataifa. Tulipata fursa ya kukutana na mwanamke aliyeathirika na virusi ambaye alijaaliwa kupata mapacha watatu waliozaliwa bila ya maambukizi. Nikiwa mjumbe wa Kamisheni  ya Umoja wa Mataifa iliyoshughulikia taarifa na uwajibikaji katika masuala ya afya ya mama na mtoto (Commission on Information and Accountability on Women’s and Children’s Health) ambayo iliendeshwa kwa umahiri na Rais Kikwete wa Tanzania na Waziri Mkuu Harper wa Canada, nina imani kwamba jumuiya ya kimataifa  hivi sasa imepata mfumo madhubuti utakaohakikisha kwamba kunakuwa na ufuatiliaji, usimamizi na uwajibikaji kuhusu afya ya mama na mtoto. Hakuna shaka kwamba mfumo huu utafikia hatua ya utekelezwaji siku za hivi karibuni.
Hali kadhalika,  kazi nzuri imekuwa ikifanywa na Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Mpango wa Uzazi Duniani (UNFPA), Babatunde Osotimehin, na Margaret Chan, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) ya kuboresha afya ya mama na mtoto. Matokeo ya jitihada  za wenzangu hawayalikuwa chachu ya utekelezaji wa majukumu ya Naibu Katibu Mkuu katika nyanja zote za maendeleo. Ama kwa hakika matunda ya kazi zao yanaimarisha imani yangu kuwa Umoja wa Mataifa ni Shirika lenye umuhimu mkubwa; na kwamba mchango wetu, japo mdogo, unasaidia sana katika kufikia malengo ya maendeleo ya milenia. Nilijawa na imani kama hiyo nikiwa katika ziara nyingine za kikazi. Kwa mfano nikiwa Montevideo,  Uruguay, Novemba 2011, pamoja na wenzangu Michelle Bachelet, Helen Clark na  Alicia Barcena, tulisimama kidete  kuunga mkono kampeni ya kitaifa ya kupiga vita vitendo vya ukatili kwa wanawake.
Nilipozuru Haiti mwezi Aprili2010, miezi michache baada ya tetemeko ambalo lilikuwa kubwa kuliko yote yaliyowahi kutokea nchini humo kwa kipindi cha takriban karne moja, nilikutana na watu ambao walikuwa wameathirika vibaya sana: waliopoteza familia nzima, waliopata ulemavu wa maisha, waliopoteza mali zao zote! Lakini bado watu hawa walikuwa na nyuso za matumaini wakitarajia mchango wa Umoja wa Mataifa na wa wadau wengine wa jumuiya ya kimataifa. Mnamo Novemba 2010 tulizuru Laos, ambako Umoja wa Mataifa unashirikiana kwa karibu na Serikali na wadau wengine wengi katika utoaji wa misaada muhimu ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kuisaidia Laos kupambana na janga la mabaki ya mabomu ya “cluster munitions”.
Hii ni mifano michache tu inayojibu hoja za wakosoaji wa Umoja wa Mataifa.Ujumbe wangu kwao ni huu: wanyonge na wenye kutaabika sehemu zote duniani ni mashuhuda na watetezi wakubwa wa Umoja wa Mataifa.  Kwa wanyonge na wahitaji walio wengi Shirika hili ni nguzo ya kutumainiwa katika jitihada zao za kila siku za kujiletea maisha yenye utu na heshima.
Mageuzi katika menejimenti na usimamizi wa mabadiliko
Ukweli huu haumaanishi kuwa Umoja wa Mataifa hauna kasoro au upungufu. La hasha! Ndiyo maana wakati wa utumishi wangu tulijielekeza kikamilifu kwenye kuboresha masuala ya utawala, uendeshaji na namna tunavyofanya kazi. Ni wazi kwamba hivi sasa Umoja wa Mataifa umebadilika kutoka chombo cha huduma za mikutano na kuwa mtendaji mwenye majukumu muhimu nje ya kumbi za mikutano. Kwa ushirikiano na msaada maridhawa wa wafanyakazi wenzangu, tulijikita katika kuhamasisha mabadiliko ya kiutendaji katika Umoja wa Mataifa, ikiwa ni pamoja na kujenga desturi ya uwajibikaji, uadilifu na kufanya kazi kwa tija zaidi huku tukitumia rasilmali chache.
Ilitubidi pia kuweka mifumo thabiti ya kusimamia mabadiliko yaliyokuwa yakijitokeza. Katika kufanya hivyo tulitambua wazi kwamba hakukuwa na njia ya mkato wala njia mbadala ya kuliimarisha Shirika letu na kulifanya liwe la kisasa zaidi katika kutekeleza majukumu yake.Tulihakikisha kwamba utendaji kazi wetu unakwenda sambamba na changamoto zilizopo, lakini pia tulizingatia ufinyu wa bajeti, misimamo tofauti  na wakati mwingine inayaokinzana ya nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa. Katika hali hii ilitulazimu kuwa wabunifu zaidi  ili  kuleta muafaka baina ya nchi wanachama na kuhakikisha kwamba raslimali chache zilizopo zinatoa tija kubwa zaidi.
Wafanyakazi ndiyo rasilmali kubwa kupita zote. Hivyo kila tulipoendelea na jitihada za kuboresha Shirika ilitubidi kuwekeza vilivyo kwa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa kwa kuwapatia fursa za mafunzo na msingi imara wa maendeleo yao kazini. Ni jambo lililo dhahiri kuwa  wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa wanatekeleza majukumu yao katika mazingira hatarishi na yenye kubadilika mara kwa mara. Tunafahamu, tena kwa uchungu mkubwa, kuwa Bendera ya Umoja wa Mataifa  –  “bendera ya bluu” –  hivi sasa si kinga tena.  Haituhakikishii usalama kwani wengi wa watumishi wetu mahiri wamekuwa wahanga wa matukio ya kikatili ya ugaidi. Nilishuhudia tukio la aina hii huko Abuja, Nigeria, ambako watumishi wenzetu walipoteza maisha kutokana na shambulio la kigaidi la tarehe 26 Agosti 2011. Na mara nyingi wenzetu wanapotangulia mbele ya haki, wapendwa wao wanaachwa katika hali ngumu ya maisha. Ni faraja kubwa kwangu kuwa miongoni mwa masuala ambayo tuliyasimamia kabla ya kumaliza utumishi wangu ni kuanzisha mchakato wa kubaini namna bora ya kuwasaidia wahanga wa majanga hayo pamoja na familia zao.
Utawala wa sheria 
 
Mojawapo ya majukumu ya Umoja wa Mataifa ni kukuza sera zinazolenga kulinda haki za binadamu na kuendeleza utawala wa sheria katika ngazi za kitaifa na kimataifa. Leo hii, nchi nyingi zimelipa kipaumbele suala  la kuimarisha utawala wa sheria, hususan kufuatia umuhimu wake katika ajenda za ujenzi wa amani (peace-building) na maendeleo stahimilivu. Kwa mantiki hiyo, nilifurahi nilipopata fursa ya kusimamia ujenzi wa mfumo madhubuti wa sera na mwongozo wa utekelezaji wa shughuli za utawala wa sheria nikishirikiana na nchi wanachama. Kwa upande wao nchi wanachama zimepanga kufanya mkutano wa ngazi ya juu wakati wa kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwezi Septemba 2012. Nia kubwa ni kuendeleza jitihada katika suala hili ili kukuza heshima ya watu wote duniani na kujenga amani kati ya mataifa.
Hitimisho
Japokuwa muda wangu wa utumishi katika Umoja wa Mataifa umefikia tamati, naamini hakuna tamati katika utekelezaji wa malengo, misingi na maadili ya Umoja wa Mataifa.  Ili mradi bado kuna umaskini duniani na mahitaji ya chakula; bado kuna changamoto ya kutunza utu na heshima ya binadamu na haja ya kuimarisha amani duniani basi hakika nitaendelea kuunga mkono jitihada, misingi na malengo ya Umoja wa Mataifa popote pale nitakapokuwa. Kwani ni dhahiri kwamba njia bora ya kukabiliana na changamoto kubwa zilizo mbele yetu ni kujenga ubia na ushirikiano wa karibu baina ya serikali, asasi za kiraia, wafanyabiashara, mashirika ya hisani, taasisi za kitaaluma na watu binafsi.
Aidha, ninaaamini kuwa vijana, kizazi ambacho kina kila sababu ya kuwa na kiu ya kuishi kwenye dunia yenye utu, usawa, haki na amani, watauchukulia Umoja wa Mataifa kuwa mbia wa kuaminika katika kujenga mustakabali wao.
Asha-Rose Migiro

Mb Dog arudi kwa kishindo, aachia ngoma mpya na kufungua studio

1 CommentBaada ya kupotea kwa muda mrefu kwenye ramani ya muziki, hatimaye Mb Dog amevunja ukimya kwa kuachia wimbo mpya uitwao ‘The Only One’ alioufanya kwenye studio yake mwenyewe aliyoifungua hivi karibuni, Makopa Inc.
Msanii huyo aliyetamba zamani na kibao ‘Latifa’ amesema kwa muda mrefu alikuwa akifanya mambo yake nchini Ujerumani na sasa ameamua kurudi kwenye game.
Katika mazungumzo ya simu aliyofanya na Bongo5, Mb Dog amesema hana wasiwasi kuwa ataishika tena mioyo ya wapenzi wa muziki wa Tannzania kwakuwa haoni kipingamizi na muziki haujabadilika sana.
“Navyoona najua muziki umechangamka katika njia zake, lakini sio kwamba watu wamebadilika kuimba na muziki utafanyika vile vile kama watu walivyozoea kuusikia, sema tu katika kuanzia kuna harakati zitakuwa tofauti muda mfupi wakati nikitulia kwasababu muda mrefu nilikuwa sijajihusisha na haya mazoezi kwasababu ya mambo yangu binafsi,” alisema.
Aliongeza kuwa ujio wake mpya unaweza kuwa zaidi ya Latifa, “hilo ni miongoni mwa mawazo niliyonayo kwasababu sijaona kama kuna vitu tofauti vinavyofanyika labda vya chinichini ambavyo sivifahamu, lakini kimuziki tu naona uko kawaida na ntafanya vizuri zaidi ya hata hivyo.”
Mb Dog amesema hajamsahau P-Funk Majani ambaye ndiye alimtambulisha kwenye muziki wa Tanzania kwa kumtengenezea hit ya Latifa. “Ujue yeye ndo kama father kwenye muziki huu, ni mtu ambaye akinifanyia kazi anatumia nguvu nyingi sana lakini sasa nimerudi, nimefanya hii ngoma mwenyewe sasabu yeye pia ana kazi nyingi, lakini kwasababu muda upo lazima niende pale kupiga ngoma mbili tatu watu waziskie kutoka pale. Katika albam yangu kuna watu muhimu kama yeye hawawezi kukosa kunipigia nyimbo.”

source:bongo5

Deidre Lorenz kukisaidia kituo cha watoto yatima cha Upendo cha Moshi

Leave a comment


Balozi wa Heshima wa mbio za Mt. Kilimanjaro Marathon katika jiji la mapesa la New York City (NYC) nchini Marekani ambaye pia ni mcheza sinema na mlimbwende maarufu kutoka jiji hilo linaloaminiwa kuwa kitovu cha pesa duniani, Mmarekani Deidre Lorenz ameahidi kukisadia kituo cha watoto yatima cha Upendo kilichopo katika Manispaa ya Moshi.

Lorenz alikitembelea kituo hicho siku mbili (tarehe 22 Juni) kabla ya kukimbia mbio za Mt. Kilimanjaro Marathon zilizotimua vumbi tarehe 24 juni mwaka huu kuanzia Moshi Club hadi Rau mudukani.

Mbio za Mt. Kilimanjaro Marathoni zilianzishwa na Marie Frances anayetoka katika jiji la matajiri la Bethesda nje kidogo ya jiji la Washingyon DC nchini Marekani mwaka 1991 baada ya kuombwa na balozi wa zamani nchini Misri.

Marie Frances aliyekuwa muandaaji wa vipindi vya television ya ABC alianzisha mbio za Pyramid Marathon zilizofana sana nchini Misri na kumfanya balozi wa Tanzania nchini Misri wakati ule kumuomba aje Tanzania kuanzisha mbio za marathon.

Mt. Kilimanjaro Marathon ilianzishwa mwaka 1991 katika Manispaa ya Moshi zikiwa ni mbio kukimbia kwa furaha (fun run) inayowaleta wazungu kupanda mlima Kilimanjaro, kukimbia na kwenda kutembelea mbuga zetu za wanyama. Mbio hizi zipo katika kiundi la Seven Continental Marathons ambazo hukimbiwa katika mabara saba ya dunia.

Deidre Lorenz ambaye amewahi kuigiza katika filamu nyingi alipatikana katika bahati nasibu (Raffle) iliyochezeshwa na Mt. Kilimanjaro Marathon 1991 wakati wa mbio za New York Marathon jijini New York Marekani mwaka 2011. Katika bahati nasibu hiyo Deidre Lorenz aliibuka mshindi na kujipatia tiketi ya bure pamoja na gharama za hoteli za kuja kukimbia mbio za Mt. Kilimanjaro Marathon mwaka huu.

Wadhamini wa mbio za Mt. Kilimanjaro Marathon ni kampuni ya ndege ya Ethiopia Airlines (ET) ambayo huwa inantoa tiketi za bei rahisi kwa wale wanaokuja kukimbia mbio hizo. ET pia hugharamia ushiriki wa Mt. Kilimanjaro Marathon 1991 katika mbio za New York Marathon, Boston Marathon na Los Angelos Marathon ili kijitangaza.

Katika mpango huo Mt. Kilimanjaro Marathon 1991 huweka banda la kutangaza vivutio vya Tanzania kama vile mlima Kilimanjaro, mbuga za wanyama, Zanzibar na mali zetu za asili.

Mkakati huu umesaidia sana kuitangaza Tanzania na hivyo kuwapa fursa watalii wengi kutoka Marekani na nchi nyingi duniani kuijua vyema Tanzania. Wengi wa wakimbiaji hawa hutembelea vivutio vya Tanzania baada ya kutembelea banda la Mt. Kilimanjaro Marathon 1991 katika mbio hizo.

Ufadhili wa Deidre Lorenz akishirikiana na taasisi ya Screen Actors Guild utakisaidia sana kituo cha watoto yatima cha Upendo ambacho kinakabiliwa na changamoto nyingi za fedha na vifaa vya kuwatunza watoto wanaolelewa kituoni hapo. Kituo hiki kilianzishwa miaka ya 60 na masista wa shirika la Precious Blood wa Kanisa Katoliki jimbo la Moshi.

Kwa miaka mingi kituo hiki kimekuwa kinapokea watoto wachanga wanaotelekezwa na mama zao baada ya kuzaliwa katika hospitali mbalimbali za mkoa wa Kilimanjaro. Kituo cha Upendo kinawapokea pia watoito ambao mama zao wamefariki wakati wa kujifungua.

Aidha Lorenz ameahidi kuwashawishi walimbwende na wacheza filamu wengine wa Marekani kuja kushiriki katika mbio za Mt. Kilimanjaro Marathon na kutembelea vivutio vya kitalii vya nchi hii kila mwaka.

source:father kidevu

Balotelli kupima ili(DNA) kujua kama ni baba wa mtoto wa Raffaella

Leave a comment


Mshambuliaji wa Manchester City na timu ya taifa ya Italia Mario Balotelli juzi ameviambia vyombo vya habari nchini Italia kuwa atachukua vipimo (paternity test) vya hospitali ili kujua kama yeye ndo baba wa mtoto ambaye mpenzi wake wa zamani anadai kuwa na ujauzito naye.
Raffaella Fico, 24, nyota wa TV na model wa nguo za ndani, aliliambia gazeti la kila wiki la Chi kuwa anategemea kupata mtoto wa Balotelli.
“Nikithibitisha kuwa mimi ndo baba, ntachukua majukumu yote,” alisema Balotelli mwenye miaka 21, kwenye maelezo yake.
“Nilifahamu kupitia kwa mtu mwingine siku chache zilizopita kuwa Raffaella ni mjamzito. Ndio maana niliamua kuwasiliana naye na hapo ndipo aliponiambia kuwa ni kweli.”
“Nimejisikia vibaya, sidhani kama ni kawaida kutoelezwa chochote mpaka mwezi wanne wa ujauzito.”
Uhusiano wa miezi 18 wa wapenzi hao ulikuwa ukizungumzwa na kuandikwa mara kwa mara kwenye vyombo vya habari vya Italia kabla hawajaachana mwezi April mwaka huu

Wema Sepetu na Diva waingia kwenye orodha ya kusaidia wasiojiweza

Leave a comment


Ray Kigosi akitoa msaada

Lady Jay Dee akitoa msaada

Lady Jay Dee

Wema Sepetu

Diva Loveness Love

Muigizaji wa filamu nchini na Miss Tanzania wa zamani (2006),Wema Sepetu anatarajiwa kwenda jijini Arusha mwezi huu na kushiriki uoashaji wa magari ili kukusanya fedha za kusaidia watu wasiojiweza jijini humo.
“On 14th July I will be in Arusha with manager kushiriki uoshaji wa magari ili kuchangia fedha za kusaidia wasiojiweza in Arusha,” alitweet jana.
Mwingine aliyeamua kujitolea nguvu na mali kuchangisha fedha kwaajili ya kuwasaidia watoto yatima ni mtangazaji wa Clouds Fm, Loveness aka Diva.
Kupitia website yake, Diva amesema, “So nimeamua kwa muda mrefu sana kutoa for charity and right now am too busy organizing this charity event inayoitwa Diva giving for charity. Aim is raising much needed funds to support orphans.
June na July imekuwa miezi iliyotumiwa zaidi na mastaa wa hapa nchini kusaidia vituo vya watoto yatima.
June 30, mwanamuziki Lady Jaydee pamoja na familia yake walikitembelea kituo cha watoto yatima cha Maunga Centre kilichopo Kinondoni jijini Dar es Salaam na kutoa misaada mbalimbali ikiwa pamoja na kushiriki chakula cha mchana na watoto hao.
Katika hotuba yake, kituo hicho kilisema kinakabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo ni pamoja na kukosa fedha za kuwalipa wahudumu, Kukosa eneo kubwa la kujenga kituo, Kukosa wafadhili, watoto kutokuwa na sare za shule na kukosa gharama za kuwasomesha (michango ya shule).
Lady Jaydee aliwaahidi kuwatafutia kiwanja kikubwa kwaajili ya kujenga kituo kingine na kusema kuwa iwapo akitokea mtu wa kuwasaidia kiwanja, watachangisha fedha za kuanza ujenzi huo.
Naye muigizaji wa filamu mwenye mafanikio makubwa nchini Raymond Kigosi aka Ray The Greatest, weekend iliyopita alikitembelea kituo hicho cha Maungo na kutoa msaada sambamba na uzinduzi wa filamu yake mpya ya Sobbing Sound.
Kupitia blog yake Ray alisema: “Hili ni jukumu la watanzania wote kuanza kuguswa katika hili maana hapa duniani sisi ni wapangaji tu makazi yetu ni kwa Mungu Baba, sasa unapopata kidogo jaribu kuwafikiria na wale waliokuwa na maisha magumu, yaani tugawane umasikini.”

source:

Older Entries

%d bloggers like this: